Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

TRC YAINGIZA SIMULATOR YA KISASA KUIMARISHA MAFUNZO NA USALAMA KATIKA UENDESHAJI RELI


news title here
27
October
2026

Wizara ya Uchukuzi imeipongeza TRC kwa kuwekeza katika teknolojia na kusisitiza umuhimu wa kuhakikisha kuwa wataalamu wanapatiwa mafunzo na kukidhi viwango vya kimataifa vya uendeshaji wa reli

Shirika la Reli Tanzania (TRC) limeendelea kuimarisha usalama wa shughuli za uendeshaji wa Reli ya Kisasa ya SGR kwa kujikita katika ununuzi wa vifaa vya kisasa na teknolojia hali ya juu utakaotoa mafunzo Kwa madereva wa treni ikiwemo ununuzi wa kifaa maalumu cha mafunzo kiitwacho 'Motion Platform Simulator ' kinachowawezesha madereva kujifunza na kufanya mazoezi ya uendeshaji wa treni katika mazingira yanayofanana na hali halisi ya reli kabla ya kuanza kazi.

Hatua hiyo inalenga kuongeza ujuzi wa wataalamu wa reli nchini, kuimarisha usalama wa abiria na mizigo pamoja na kupunguza gharama za mafunzo na matengenezo ya treni yanayotokana na makosa ya kiutendaji.

Akizungumza Oktoba 27, 2026, wakati wa kuhitimisha ziara ya kikazi ya ukaguzi wa mradi wa SGR kuanzia kipande Cha 3- 6 Cha ujenzi wa SGR eneo la Fela Jijini Mwanza, Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa Mnyaa, ameipongeza TRC kwa kuwekeza katika teknolojia hiyo na kusisitiza umuhimu wa kuhakikisha kuwa wataalamu wanapatiwa mafunzo na kukidhi viwango vya kimataifa vya uendeshaji wa reli.

Waziri huyo amesema Serikali imewekeza fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu ya SGR na ununuzi wa vifaa vya kisasa, hivyo ni muhimu uwekezaji huo kulindwa kwa kuhakikisha kunakuwepo na mifumo madhubuti ya matengenezo, mafunzo ya wataalamu na uendeshaji salama wa treni.

Mhe.Waziri amefafanua kwamba kifaa hicho kina uwezo wa kumwezesha dereva kufanya mazoezi ya kuongeza au kupunguza mwendo, kutumia breki za dharura, kukabiliana na hali mbaya ya hewa, kutambua changamoto za njia na kujifunza namna ya kupita katika mikunjo ya reli pamoja na maeneo yenye mifumo ya kubadilishia njia za treni.

Aidha, ameitaka TRC kuhakikisha inawaandaa wakufunzi wenye sifa zinazotambulika kimataifa kwa kushirikiana na taasisi za mafunzo ya reli duniani na vyombo husika vya uthibitishaji wa taaluma ili madereva wanaohitimu waweze kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia viwango vinavyotakiwa.

Kwa namna nyingine Waziri Mbarawa amesisitiza umuhimu wa kuanzisha utaratibu wa mara kwa mara wa kuwarejesha madereva kujifunza kwenye kifaa hicho kwa ajili ya mafunzo ya nyongeza na tathmini ya uwezo kama wanavofanya marubani wa ndege na fani nyingine za udereva ili kuhakikisha wanaendelea kuendana na teknolojia na viwango vya usalama katika sekta ya reli.

Vilevile, Waziri amependekeza TRC kutumia uwekezaji huo kama msingi wa kuanzisha kituo cha ubora (Centre of Excellence) katika mafunzo ya reli kitakachokuwa na vifaa vya kisasa, karakana na miundombinu ya kutosha kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa Watanzania na wataalamu kutoka nchi nyingine Afrika na duniani.

Katika kuhitimisha kwake ziara ya siku nne ya kukagua ujenzi wa SGR vipande vya tatu, vinne, sita na tano Waziri amesema ziara imeonesha maendeleo mazuri katika baadhi ya maeneo, huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza kasi ya utekelezaji wa maeneo ambayo bado yanahitaji juhudi zaidi.

Ameeleza kuwa ujenzi wa kipande cha tano, kinachoanzia Isaka - Mwanza , kimefikia takribani asilimia 69.77 za ujenzi , huku kipande cha sita( Tabora - Kigoma) nacho kinaendelea vizuri na matarajio ya kukamilika ifikapo mwaka 2028, sambamba na kuimarisha mikakati ya kuhakikisha vipande vya tatu na vinne vinakamilika kwa wakati.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu Shirika la Reli Tanzania Mha.Machibya Shiwa amesema TRC inaendelea na utekelezaji wa mipango ya ununuzi wa vifaa na mitambo ya kisasa kwa ajili ya matengenezo ya miundombinu ya reli na kuimarisha shughuli za uendeshaji.

ambapo Uwekezaji huo unajumuisha pia ununuzi wa vichwa vya treni za umeme, treni za abiria na vifaa vingine vinavyohitajika katika uendeshaji wa mtandao wa SGR.

Mha.Machibya ameongeza kuwa TRC inaendelea kuweka mkazo katika maendeleo ya miundombinu, teknolojia na rasilimali watu ili kuhakikisha uwekezaji wa Serikali katika reli unaleta manufaa yaliyokusudiwa kwa wananchi, biashara na uchumi wa Taifa.

Ikumbukwe TRC inaazimia kuwa na Wafanyakazi wenye uwezo wa hali ya juu na ufanisi katika utendaji kwani Wafanyakazi ambao hawana ufanisi haswa madereva wanaweza kuongeza gharama ya kuharibika miuondombinu na matengenezo ya gharama kubwa ya mara Kwa mara.