Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

TRC YAENDELEA NA ZOEZI LA ULIPAJI FIDIA ILI KUPISHA MRADI WA UJENZI WA RELI YA KISASA MOROGORO - MAKUTUPORA


news title here
06
October
2019

Shirika la Reli Tanzania - TRC laendelea na zoezi la ulipaji wa fidia na kifuta machozi ili kupisha ujenzi wa reli ya kisasa - SGR kwa awamu ya pili Morogoro - Makutupora hivi karibuni Oktoba 2019.

Zoezi hilo linaendelea katika Halmashauri ya jiji la Dodoma katika mtaa wa Ihumwa ambapo zaidi ya wananchi elfu mbili watapatiwa fidia ya majengo, mashamba na viwanja pamoja na vifuta machozi kwa ndugu wa marehemu ambao makaburi yao yamehamishwa.

Katika zoezi hilo lililofunguliwa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Mhe. Patrobas Katambi, Mkuu wa Wilaya amewataka wananchi wanaopatiwa fidia kuzitumia katika mambo yenye maslahi ikiwemo kujenga nyumba nzuri na za kisasa kwa kufuata taratibu kwa kuwa eneo la Ihumwa ni la kimkakati.

Aidha maeneo mengine yatakayo patiwa fidia hizo ni pamoja na Chilwana, Kikombo na Chololo, Chamwino, Igandu, msamalo na Mnase.

Mhe. Katambi amesema kuwa wananchi wanapaswa kuwekeza na kuangalia mipango mizuri ya kifedha ili kuweza kujikwamua kiuchumi kwa kupata maelekezo na ushauri wa kitaalamu wa ujenzi kutoka kwa wataalam kuanzia ngazi za vijiji kuendana na mipango miji.
“Mnalipwa fedha hizi nyingi hivyo msizitumie vibaya, mjiwekee misingi na mikakati ya utumiaji wa fedha hizi", alisema Mhe. Katambi

Vilevile Mhe. Katambi ameongeza kuwa Jiji la Dodoma litanufaika sana kutokana na mradi wa SGR kwa kurahisisha usafirishaji ambao utakuza biashara na mzunguko wa bidhaa kwa ujumla pia amewaasa wananchi kulipa kodi ipasavyo hasa kutoa na kupokea risiti pindi wanapouza au kununua bidhaa au huduma ili kuzidi kuingiza mapato serikalini.

Naye Meneja msaidizi Mradi wa SGR Morogoro - Makutupora Mhandisi Christopher Mang’wela amesema kuwa Shirika limezingatia fidia ambayo ni ya haki kamilifu inayozingatia wakati hivyo wananchi wanatakiwa kufanya mambo ya maendeleo kama kujenga nyumba za kisasa pamoja na kuwekeza katika kilimo kwa manufaa ukuzaji uchumi wa Taifa.
“Tuzitumie fedha hizi kwa kufanya yale yaliyotarajiwa na si vinginevyo", alisema Mhandisi Mang’wela