TRC YAENDELEA NA ZOEZI LA FIDIA MKOANI MWANZA NA SHINYANGA KUPISHA UJENZI WA KAMBI ZA SGR
May
2021
Shirika la Reli Tanzania – TRC laendelea na zoezi la ulipaji fidia ili kupisha ujenzi wa kambi za Mradi wa reli ya Kisasa – SGR katika maeneo ya Fela, Bukwimba, Malampaka mkoani Mwanza na Didia mkoani Shinyanga Mei 17, 2021.
Zoezi hilo linaendelea chini ya usimamizi wa Maafisa kutoka TRC wakishirikiana na maafisa kutoka Wilaya husika mkoani Shinyanga na Mwanza ambapo Mei 17, 2021 zoezi limeendeshwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga tarafa ya Ikungwi katika kijiji cha Didia ambapo wananchi 20 wamepokea hundi za malipo ya fidia.
Aidha, ulipwaji wa fidia unakwenda sambamba na maandalizi ya uzinduzi rasmi wa Mradi huo kipande cha Mwanza – Isaka chenye urefu wa KM 341, ambapo mara baada ya uzinduzi huo kufanyika hivi karibuni shughuli za ujenzi wa reli ya kisasa zitaanza rasmi na kuwawezesha wananchi kuanza kunufaika na mradi huo.
Mradi wa SGR Mwanza – Isaka unapita katika mikoa ya Mwanza na Shinyanga ambapo kwa hatua za awali tayari wananchi wa maeneo ya Fela, Didia. Malampaka na Bukwimba ambayo kambi za mradi huo zitajengwa wameendelea kupokea fidia ili kupisha ujenzi wa kambi za mradi huo.
Wananchi wa maeneo hayo ambao wamepatiwa fidia zao wameridhishwa na zoezi hilo ambapo wameeleza kuwa fidia hizo zimelipwa kwa wakati na wamefurahishwa kwa kuwa ahadi iliyotolewa na Serikali kwa kila mwananchi ambaye eneo lake limepitiwa na mradi kulipwa fidia anayostahili imetimizwa.
Mradi wa SGR Mwanza – Isaka unatarajiwa kuzalisha jumla ya ajira za moja kwa moja zaidi ya 11,000 zitazalishwa na zisizo moja kwa moja zaidi ya 55,000 na utachochea ukuaji wa uchumi kwa kuvipatia nafasi viwanda vya ndani fursa ya kuuza malighafi za ujenzi.