Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​TRC YAENDELEA NA UTATUAJI WA CHANGAMOTO KWA JAMII INAYOISHI KARIBU NA ENEO LA MRADI WA SGR


news title here
10
May
2021

Shirika la Reli Tanzania – TRC kupitia Wataalam wake kutoka vitengo mbalimbali kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa mpaka ngazi ya Vijiji wameendesha zoezi la kufanya tathimini za athari na changamoto zilizojitokeza kwa wananchi walio katika maeneo ambayo ujenzi wa reli ya kisasa –SGR unaendelea, Mkoani Morogoro hivi karibuni Mei, 2021.

Zoezi lilianzia Mkoani Dar es Salaam, Ilala mpaka Morogoro ambapo lengo kubwa la zoezi hilo ni kupita katika maeneo yote sambamba na kutatua changamoto na malalamiko yote ambayo Shirika la reli lilipokea kutoka kwa wananchi ambao wameathirika na mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa – SGR kipande cha kwanza Dar es Salaam – Morogoro.

Aidha, zoezi hilo limejikita hasa katika kutatua changamoto ambazo wananchi zimewapata kutokana na ujenzi wa reli hasa wananchi waishio maeneo hatarishi, wananchi wanaoshindwa kupata huduma za kijamii, kuhakiki wananchi ambao wameshalipwa fidia kama wameachia maeneo na kusikiliza malalamiko ya ardhi na fidia pamoja athari za mazingira wanazokutananazo wakati wa utekelezaji wa mradi huo.

Kwa upande wake Mhandisi Rajab Mahaja kutoka TRC, amabaye ni Mkuu wa wataalam hao, amaeeleza namna zoezi lilivyoendeshwa kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zote katika kutatua changamoto za wananchi huku idadi kubwa ya wananchi waliokuwa wakilalamika kutokurizika na ulipwaji wa fidia na ardhi ikiwa ni ukosefu wa elimu ya kutosha hasa katika mambo ya ulipaji fidia na utwaaji wa ardhi na mara tu baada ya wananchi kupewa elimu waliridika na kuona hakuna ambacho wanadai kutoka kwa Shirika la Reli Tanzania.

“Tumefika katika maeneo yote tukafanya tathimini, baadhi ya wananchi waliokuwa wakilalamika na kusema Shirika limewapunja fidia tuliamua kuwapa elimu ya namna zoezi la uthamini linavyofanyika wengi walielewa na baada ya kuoneshwa jedwali la uthamini waliona kabsa hawana ambacho wanadai kwa Shirika” alisema Mhandisi Mahaja.

Hata vivyo Mhandisi Mahaja aliongeza kuwa, elimu waliyoitoa kwa wananchi imeleta manufaa chanya kwao na kwa Serikali kwa ujumla kwa sababu viongozi wa Serikali walio katika maeneo hayoo wamekuwa wakisumbuliwa sana na wananchi kwa madai ya kuwa Shirika halijawapa fidia stahiki. Hivyo kupitia elimu waliyopewa kabla ya kuanza kutatua changamoto wananchi wameweza kuona namna Shirika lilivyofuata Sheria ya ardhi na fidia katika kutwaa maeneo yao.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Mahaja ameeleza kuwepo kwa vitendo vya ukaidi kwa baadhi ya wananchi ambao tayari wamekwisha kulipwa fidia lakini bado hawajaondoka na baadhi yao kubomoa nyumba upande mmoja na kuendelea kukaa katika maeneo hayoo na wengine kupangisha hivyoo alitoa wito kwa wale wote wanaoendelea kukaidi watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Naye Bi. Lightness Mngulu Mtaalam wa Masuala ya Kijamii – TRC, amebainisha kuwa zoezi la kupita na kuona changamoto zinazoikumba jamii iishiyo eneo la mradi ni jambo ambalo limeleta afya kwa jamii husika lakini pia kwa Shirika la Reli, kutokana na kwamba kwa muda mrefu wao kama wataalam wa mambo ya jamii wamekuwa wakipokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi, hivyo kitendo cha Shirika kujitokeza na kutatua changamoto na zingine kuzipeleka ngazi za juu ni jambo la muhimu kwa jamii na inaonesha uwajibikaji chanya wa Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania .

“Tumekuja kutatua changamoto pamoja na malalamiko yote angalau tuweze kuona namna ya kuweza kuwarudishia maisha yao kama ilivyokuwa awali. Kupitia zoezi hili tutakuwa tumepunguza kwa asilimia kubwa malalamiko ambayo yalitufikia na kuna mengi hayakutufikia wananchi walibaki nayoo na kuendelea kulalamika lakini baada ya kukutana na wananchi wa maeneo haya tumeweza kuyabaini na kuyatafutia ufumbuzi chanya kwa kufanya hivyo tutakuwa tumewatendea haki wananchi na wataufurahia mradi wao” alisema Bi Lightness.