Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​TRC YAENDELEA KUTOA ELIMU YA ULINZI WA MIUNDOMBINU YA RELI (SGR) DODOMA


news title here
22
March
2024

Maafisa kutoka TRC kwa kushirikiana na viongozi wa Serikali wameanza zoezi la kutoa elimu kwa wananchi mkoani Dodoma kuhusu zoezi la uwashaji wa umeme katika mradi wa reli ya kiwango cha kimataifa - SGR katika kipande cha pili Morogoro - Makutupora, Machi 2024.

Zoezi litafanyika katika maeneo ya Dodoma Mjini, Makulu, Tambuka Reli, Kilimani, Kikuyu Kusini, Chamwino na Mpwapwa.

Mkuu wa wilaya ya Dodoma Alhaji Jabir Mussa Shekimweri ameishukuru TRC kwa kuandaa zoezi la utoaji elimu kwa wananchi juu ya zoezi la uwashaji wa umeme na kulinda miundombinu ya reli katika kipande cha pili Morogoro - Makutupora.

"Nawashauri kutumia redio za ndani katika mkoa wa Dodoma pamoja na TV Dodoma na muandae vipeperushi kwaajili ya kuelimisha jamii Ili tuweze kusikika na kueleweka zaidi kwa wananchi" alisema Alhaji Mussa Kimweri.

Mhandisi wa Umeme kutoka TRC Godlove Nassary amesema katika ujenzi wa kipande cha pili Morogoro - Makutupora wamefikia hatua ambayo Mkandarasi anataka kuwasha umeme katika mfumo wa nyaya zilizotandazwa juu ya reli (Catenary System).

"Tangu mnamo tarehe 8 Machi 2024 vituo vya kupoza umeme vilivyounganishwa kwenye gridi ya taifa (TPS) vimewashwa, pamoja na Transfoma kubwa za kupoza umeme kutoka msongo wa 220,000V mpaka 27,500V na kwa sasa mkandarasi anakamilisha kujaribu vituo vya umeme vilivyo kando ya reli" ameongeza Mhandisi Nassary.

Pia Mhandisi Nassary amesema kuwa mwanzoni mwa mwezi wa nne 2024 Mkandarasi anatarajia kuruhusu umeme katika mfumo wa nyaya zilizojengwa juu ya reli ya SGR hivyo Shirika linawaomba wananchi kuchukua tahadhari kwani umeme wa 27,500V utakuwa ukipita katika nyaya hizo, pia vyuma vya reli pamoja na nguzo za chuma zilizopo pembezoni mwa reli sio salama kushika au kukaa.

"Tunaomba mtu akipita juu ya reli asipite amebeba kitu kirefu kinacho karibia kugusa waya wa umeme, endapo mtu atajaribu kugusa waya wa umeme, vyuma vya reli au nguzo za chuma yupo katika hatari ya kuweza kupigwa shoti na kupoteza maisha" amesisitiza Mhandisi Nassary.

Zoezi la utoaji elimu kutoka kwa maafisa wa TRC kwa kushirikiana na viongozi wa Serikali kwa wananchi juu ya uwashaji umeme kwenye mradi wa SGR ni endelevu kwenye maeneo yote ambako reli ya kisasa imepita na wananchi wanaombwa kuendelea kujitokeza kwa wingi kwenye mikutano itakayokua inafanyika katika ofisi za Serikali za mitaa, vijiji na kata kwaajili ya kupata elimu.