Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​TRC YAENDELEA KUSISITIZA WANANCHI KUHUSU UTUNZAJI WA MIUNDOMBINU YA RELI


news title here
05
December
2024

Shirika la Reli Tanzania - TRC kupitia kitengo cha Habari na Uhusiano kwa kushirikiana na watalaamu mbalimbali kutoka TRC pamoja na viongozi wa serikali za mtaa, vijiji na ofisi ya Mkuu wa mkoa na Wilaya Morogoro limeanza kufanya kampeni ya uelewa kwa wananchi juu ya utunzaji wa miundombinu na usalama wa reli kwa wananchi mkoani Morogoro tarehe 05, Disemba 2024.

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Dkt. Rozalia Rwegasira amesema usafiri wa treni ya mwendokasi umekua chachu katika mkoa wa Morogoro kwani mkoa huo unapokea wageni wengi kila siku kwaajili ya shughuli za kitalii na kibiashara na hii inautengenezea mapato mkoa wa Morogoro.

Dkt. Rozalia ameipongeza TRC kwa kuandaa zoezi la uelemishaji kuhusu utunzaji wa miundombinu ya reli katika halmashauri ya Manispaa na Halmashauri ya wilaya ya Morogoro katika maeneo yote ambako reli ya SGR imepita.

"Watu wanaohujumu huu mradi ikiwemo kuiba nyaya na kukata fensi napenda kutoa rai hivyo vitendo havikubaliki kwani vinarudisha nyuma maendeleo ya nchi katika sekta ya usafirishaji" amesisitiza Dkt. Rozalia.

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro pia amewaagiza viongozi wa kata, vijiji na mtaa katika vikao vyao waongeze na ajenda ya elimu ya utunzaji wa miundombinu ya reli kwa wananchi pamoja na miradi mingine ya maendeleo inayofanywa na Serikali nchini.

Afisa Uhusiano kutoka TRC Bi. Amina Juma Warisanga amesema kuwa dhumuni la kampeni ni kujenga uelewa na kushirikisha wananchi katika ulinzi na usalama wa miundombinu ya reli.

Bi. Warisanga ameongeza kua awamu ya kwanza ya kampeni hii inafanyika mkoa wa Morogoro, Pwani na Dar es Salaam ambapo Morogoro imefanyika Morogoro manispaa katika mitaa ya Azimio na Kihonda kaskazini kata ya Kihonda na zoezi hili litaendelea Tungi na Kinguluira Morogoro manispaa na kampeni hii itafanyika Morogoro vijijini - Pangawe, Mikese, Ngerengere na Kidugalo.

Afisa msaidizi wa ulinzi na usalama wa Reli Rajabu Kasongo amesema reli ya SGR inatumia umeme mkubwa hivyo sio salama kwa wananchi kukatiza maeneo ambayo sio rasmi kwaajili ya kuvuka reli. Pia amesisitiza shughuli zote za kibinadamu ikiwemo ufugaji, kulima na biashara zifanyike nje ya hifadhi ya njia ya reli.

"Napenda niwakumbushe wananchi Sheria ya Reli namba 10 ya 2017 inakataza kuhatarisha usalama wa reli na watumiaji wa reli, uvamizi na kuingia bila ruhusa kwenye maeneo ya Reli na wizi. Sheria ya kanuni ya adhabu namba 16 R.E 2019 inakataza aina yoyote ya uharibifu wa miundombinu ya reli, na Sheria ya uhifadhi wa mazingira 2004 inakataza uharibifu na uchafuzi wa mazingira, kwahiyo ni jukumu la kila mwananchi kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira yanayozunguka jamii pamoja na uhifadhi wa reli kwa ujumla", amesisitiza Kasongo.

Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa Azimio kata ya Kihonda, Morogoro Manispaa Bwana Moses Denge amesema wananchi wa mtaa wa Azimio wapo bega bega kwa TRC katika kuhakikisha miundombinu ya reli inalindwa na usalama wa reli ya SGR unakua salama.

"Tupo tayari kutoa ushirikiano mkubwa katika kuilinda reli yetu ili miundombinu iwe salama kwani inaturahisishia usafiri" ameongezea Mwenyekiti Denge.

Shirika la reli Tanzania linaendelea na utoaji wa huduma za usafiri wa treni za abiria SGR pamoja na reli ya zamani (MGR) na linaendelea na usimamizi wa ujenzi wa mradi wa SGR Makutupora - Tabora, Tabora - Isaka, Isaka - Mwanza na Tabora - Kigoma.