Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​TRC YAANZA KUTOA ELIMU YA UELEWA KUHUSU ULINZI NA USALAMA WA RELI JIJINI ARUSHA


news title here
04
August
2020

Shirika la Reli Tanzania – TRC limeanza kampeni ya uelewa itakayofanyika kwa siku saba ikiwa ni muendelezo wa mpango wa kuelimisha umma kuhusu ulinzi na usalama wa miundombinu ya reli kwa wananchi katika mikoa ya Arusha, Moshi na Tanga, kampeni hiyo imeanza rasmi Agosti 3, 2020.

Kampeni hiyo imelenga kuwaelimisha wananchi wote pamoja na wanaoishi au kufanya shughuli za kiuchumi na kijamii karibu na maeneo ya reli kuhusu matumizi sahihi ya alama za usalama wa reli pamoja na namna ya kushiriki kikamilifu katika kudhibiti hujuma na vitendo vyote vinavyoweza kupelekea ajali na uharibifu katika njia ya reli.

Kampeni imejumuisha wataalamu kutoka Idara mbalimbali ikiwemo Idara ya Uendeshaji, Ujenzi na Miundombinu, Udhibiti wa Ajali, Masuala ya Kijamii na Kitengo cha Habari na Uhusiano ambapo sambamba na kampeni hiyo wataalamu wa njia wanafanya ukaguzi wa reli kipande cha Arusha – Moshi kwa ajili ya kujiridhisha na ubora na usalama wa njia hiyo kabla ya kuanza rasmi kwa safari za treni hivi karibuni.

Aidha, timu ya mawasiliano kutoka TRC inatoa elimu hiyo na kuhamasisha wananchi kupitia vyombo vya Habari vilivyopo mkoani Arusha, Moshi na Tanga pamoja na kufanya mikutano ya ana kwa ana na wananchi wanaoishi au kufanya shughuli za kiuchumi na kijamii katika maeneo yaliyo karibu na reli.

Shirika linaendelea kuwasisitiza wananchi wa mikoa ya Arusha, Moshi na Tanga kuwa linaendelea kuboresha huduma za usafiri wa reli kwa kufufua njia za reli zilizokufa ikiwemo reli ya Moshi - Arusha hivyo wanapaswa kutambua kuwa wana jukumu la kuhakikisha miundombinu ya reli inakuwa salama muda wote ili kudhibiti ajali zinazoweza kusababisha uharibifu.