TRC, TIGO WAADHIMISHA WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA

October
2024
Shirika la Reli Tanzania - TRC kwa kushirikiana na kampuni ya mitandao ya simu ya TIGO wamefanya hafla fupi ya kuadhimisha wiki ya huduma kwa wateja katika jengo la stesheni ya SGR jijini Dar es Salaam Oktoba 9, 2024.
Wiki ya huduma kwa wateja imeanza siku ya tarehe Oktoba 7, 2024 na kutarajiwa kumalizika mnamo tarehe Oktoba 11, 2024 yenye kauli mbiu inayosema “Huduma zenye ubora na za kiwango cha juu zaidi”.
Mkurugenzi Mkuu wa TRC Ndugu Masanja Kadogosa alieleza kuwa ni furaha kubwa kwa TRC kushirikiana na TIGO kuadhimisha wiki ya huduma kwa wateja kwa kutegemeana kibiashara na kuona umuhimu wa wateja.
“Watu pamoja na kwamba wanauhitaji wa kusafiri na treni ila kama hawapati huduma nzuri kazi yote ikaonekana ni bure” alisema Ndugu Kadogosa.
Ndugu Kadogosa alisema kuwa jinsi mteja anavyopokelewa na kupatiwa huduma nzuri ndivyo shirika litakavyozidi kukua bila kulinganisha uzuri wa reli na treni.
“Muonekano, namna ya kuzungumza, kutembea na kuangaliana na mtu vinaleta thamani sababu bila ya huduma nzuri kwa wateja kunakua kama hakuna kinachotendeka” alisisitiza ndugu Kadogosa.
Ndugu Kadogosa aliongezea kuwa TRC kwa kuendelea kuthamini haja ya wateja wao kwa kushirikiana na TIGO mteja anaweza kukata tiketi mtandaoni na kulipia kupitia Tigo Pesa.
Pia Ndugu Kadogosa alielezea sera ya “Open Access “ ambayo inalengo la kumuwezesha mteja kupata huduma ya kutumia reli kwa kutumia treni zao kusafirisha mizigo.
“Hivi karibuni tulipata tuzo kama taasisi bora ya umma ambayo inashirikisha wananchi na kuwahabarisha kwa ufasaha na haraka hivyo huu ni mfano kwa kua taasisi inayotoa ushirikiano na huduma nzuri kwa wananchi” alisema Ndugu Kadogosa.
Naye Afisa Mkuu Tigo Pesa Bi. Angelica Pesha alisema kuwa kampuni ya TIGO inaelewa kuwa usafiri ni muhimu hivyo ni vizuri kuwa na ushikiano huo na TRC ili kumuwezesha mteja kulipia tiketi kirahisi kupitia Tigo Pesa.
“Ushirikishwaji wa kifedha ni nguzo muhimu kwa kila mwananchi ili kumrahisishia kufanya malipo kiusalama zaidi popote ulipo na kuepukana na kukaa foleni ya kupata tiketi” alisema Bi. Angelica.
Shirika la Reli Tanzania linalenga kuboresha utoaji wa huduma kwa kuzingatia sheria, kanuni na ubora wa huduma zinazotolewa na TRC na pia kuendelea kushirikiana na TIGO ili kuwapa urahisi wateja na kuendelea kuchangia pato la taifa.