Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

SHIRIKA LA RELI TANZANIA LIMEENDELEA KUFANYA UELIMISHAJI KWA JAMII KUHUSU UHAMISHAJI MAKABURI


news title here
21
August
2020

Shirika la Reli Tanzania – TRC limeendelea kufanya mazungumzo na viongozi wa Serikali kwa ngazi ya wilaya, Vijiji na Kata pamoja na wananchi walengwa. Mazungumzo hayo yamelenga kuwaelimisha wananchi kuhusu utaratibu na namna zoezi la kuhamisha makaburi utakavyo endeshwa, ili kupisha ujenzi wa miundombinu ya umeme itakayotumika kuendesha treni ya umeme punde itakapokamilika. Mazungumzo hayo yamefanyika katika vijiji vya Mikese, Mtego wa simba, Kidugalo na Pangawe, Mkoani Morogoro hivi karibuni Agosti, 2020.

Mazungumzo hayo yamefanyika na viongozi mbalimbali na wataalamu wa fani mbalimbali ngazi ya wilaya akiwemo, Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Usalama Wilaya, Afisa ardhi wilaya, Afisa afya Wilaya, na viongozi wa vijiji na kata. Kikao hicho kilikuwa na lengo la kuwaelimisha wananchi kuhusu utaratibu utakao tumika kuhamisha makaburi kutoka eneo lililopitiwa na miundombinu ya umeme pamoja na malipo ya kifuta machozi kwa wananchi walio hamishiwa makaburi ya ndugu zao.

Zoezi la kuhamisha makaburi linatarajiwa kuanza rasmi Agosti 18, 2020 katika kijiji cha Kidugalo na baadae kuendelea kwenye vijiji vingine ambapo jumla ya makaburi 342 yanatarajiwa kuhamishwa kupisha ujenzi wa njia ya umeme na tayari maeneo ya kuhamishiwa yamekwisha kutengwa na Serikali ya vijiji husika.

Aidha, mazungumzo hayo baina ya Serikali na wananchi yalijikita hasa katika kutoa elimu ya uelewa kwa wananchi kabla ya zoezi kuanza ili kufanya zoezi kuwa rahisi na hatimaye kufikia lengo. Elimu hiyo ilihusu umuhimu wa kuondoa makaburi katika mradi, malipo ya kifuta machozi, ushirikishwaji wa viongozi wa dini na mila katika zoezi. Mara baada ya vikao kuisha Serikali ya kijiji na watendaji wa TRC wakishirikiana na viongozi wa wilaya walielekea eneo la makaburi ili kuona makaburi hayo na kukagua eneo yatakapo hamishiwa.

Naye mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Bw. Hilary Sagala Ametoa wito kwa Serikali za vijiji na ndugu wa marehemu kutoa ushirikano wakutosha ili kuhakikisha zoezi linaenda vizuri na hatimaye kukamilika na mkandarasi kuendelea na ujenzi wa reli ya kisasa ambayo itakuwa ni mkombozi wa uchumi kwa wananchi waishio maeneo ya pembezoni mwa reli.

“Sisi kama Serikali ya Wilaya tunatoa wito kwa watendaji wote pamoja wananchi kutoa ushirikiano kwa Shirika la Reli katika zoezi hili zito ambalo tunatarajia kuanza hivi karibuni. Tunatambua kuwa zoezi la kuhamisha makaburi lina taratibu zake, Hivyo tuhakikishe mila na imani za Marehemu zinazingatiwa viongozi wote wa dini watakuwepo kwa ajili ya mazishi” Bw. Sagala alisema.

Katika hatua nyingine, Mtaalamu wa mambo ya jamii na mazingira TRC Bi. Anisia Rumwisha amezungumzia vipaumbele wanavyozingatia katika swala zima la uhamishaji makaburi, kuwa ni uelimishwaji wa jamii, utu sambamba na mila na desturi pamoja na imani huwa vinazingatiwa kabla na baada ya zoezi. Bi Anisia ameongezea kuwa wao kama wataalamu wa mambo ya jamii wanauwezo wa kuongea na wananchi hasa kwa kutumia taaluma zao ili wananchi waweze kuelewa.

“Zoezi kama hili linahitaji kuelimishwa kwa umakini na upole lakini pia kuwatia moyo kwa sababu unakuwa umeamsha majonzi yaliyokuwa yamepita, nahili zoezi lazima tulifanye na wananchi ili kupata matokeo chanya” Bi. Anisia alisema.