Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​SHIRIKA LA RELI TANZANIA LAZINDUA MFUMO WA UKATAJI TIKETI KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI


news title here
04
April
2020

Shirika la Reli Tanzania – TRC lazindua rasmi mfumo mpya wa ukataji tiketi kwa njia ya kielekroniki katika hafla fupi iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo ofisi ya Makao Makuu ya Shirika jijini Dar es Salaam Aprili 4, 2020.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Mgeni rasmi Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Isack Kamwele, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TRC Prof. John Wajanga Kondoro, Kaimu Mkurugenzi Mkuu Ndugu Focus ,Mwakilishi kutoka Mamlaka ya Serikali Mtandao Bwana Benedictor Ndomba, Mkurugenzi wa huduma za Tehama, Menejimenti ya TRC, wafanyakazi na wanahabari.

Waziri Kamwele amesema kuwa TRC imetekeleza agizo la serikali ya awamu ya tano kwa kuwa kila shirika la serikali linatakiwa kuwa na mfumo mpya wa malipo wa kielektroniki na amefurahishwa sana na hatua hii iliyofikiwa na TRC ya kuwa na Mfumo wa kukusanya mapato, ninaimani Shirika litaimarisha uendeshaji wake ili kupunguza matumizi, kuongeza ufanisi pamoja na kuongeza mapato.

“Serikali ya awamu ya tano imekua ikielekeza TRC kuhusu umuhimu wa matumizi ya teknolojia ili kuboresha huduma na kuongeza ufanisi wenye tija hasa katika ukusanyaji wa mapato ya kielektroniki” alisema Mhe. Kamwele.

Pia Mhe. Kamwele amelipongeza Shirika la Reli Tanzania kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao –EGA kutekeleza agizo hilo la serikali na kutengeneza mfumo wa tiketi wa kielektroniki (E-Ticket) na usimamizi wa mizigo kwa njia ya mtandao (E-Cargo) .

“Leo tumekusanyika kushuhudia uzinduzi rasmi wa mfumo huu ambao utaondoa kabisa matumizi ya tiketi za kuandika kwa mkono, kiukweli ninawapongeza sana TRC na EGA” alisema Mhe. Kamwele.

Hata hivyo Mhe. Kamwele amesema kuwa kwa mwaka 2017/2018 kabla ya matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa tiketi, TRC ilikua ikikusanya mapato ya Shilingi 39.7 Bilioni na baada ya kuanza kwa matumizi ya mfumo huu mapato yameongezeka na kufikia kiasi cha Shilingi 44.7 Bilioni kwa mwaka 2018/2019.

Aidha, kwa Upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TRC Prof. John Kondoro amemshukuru Waziri kwa ujio wake pia aliongeza kuwa miongoni mwa maagizo aliyotoa Disemba mwaka 2019 ni pamoja na kuanzisha mfumo wa kielektroniki wa kukata tiketi na ambao hivi sasa umekamilika na umeanza kufanya kazi .

Uongozi wa Shirika la Reli Tanzania wamefurahishwa na utekelezaji uliyofanywa na watumishi wazawa ambao ni watumishi kutoka TRC na EGA na kupelekea kupunguza gharama za utengenezaji mfumo kwani Shirika imetumia fedha kidogo kuliko kutoa tenda kwa kampuni binafsi.

Akiongea katika Uzinduzi huo Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania –TRC Ndugu Focus Sahani alisema mfumo huo wa kielectroniki utasaidia katika ukusanyaji mapato ya shirika kwani kabla ya mfumo shirika lilikuwa linakusanya mapato ya kiwango kidogo lakini tangu mfumo uanze katika kipindi cha majaribio Shirika limekusanya mapato zaidi kuliko awali, aliongeza kuwa mfumo una faida nyingi hasa katika kipindi hiki cha mlipuko wa ugonjwa wa ‘Corona’ shirika litaweza kusimamia vizuri agizo la serikali la ’level seat’ na kupunguza mikusanyiko katika maeneo ya kukata tiketi.

Mkurugenzi wa Teknolojia ya Mfumo wa Mawasiliano (Tehama) TRC Senzige Kisenge amesema “ukiwa na kifaa chochote kinachopokea mtandao wa ‘Internet’ unatembelea Tovuti TRC utapata maelekezo na utaweza kupata tiketi yako, hatua ni rafiki na rahisi hivyo tunaomba ushirikiano kutoka kwa wateja wetu”.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa huduma za TEHAMA kutoka EGA Bwana Benedict Ndomba kutoka, amesema “EGA ina wajibu wa kuhakikisha matumizi ya TEHAMA Serikalini yanakuwa bora ili kuboresha utoaji huduma kwa umma, tuliwasiliana na TRC 2018 wakaona kuna eneo la TEHAMA inabidi liboreshwe eneo hilo ni uuzaji wa tiketi au ununuzi wa tiketi za abiria na mizigo tulifanya nao kazi na mfumo umefanyiwa majaribio katika vituo 71 na mpaka kufika leo tumeona umeweza kuzinduliwa rasmi, mfumo umefanyiwa majaribio kwa zaidi ya mwaka na tumejiridhisha sasa unaweza ukatumika”.