Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

SHIRIKA LA RELI TANZANIA LAONGEZA SAFARI ZA TRENI ZA ABIRIA MSIMU WA SIKUKUU ,KWA NJIA YA KASKAZINI


news title here
20
December
2023

Shirika la Reli Tanzania limeongeza safari za treni za abiria zinazofanya safari kutoka Dar Es Salaam kuelekea mikoa ya kaskazini Tanga , Moshi na Arusha hivi karibuni , Disemba 19 , 2023 .

Kuongezwa kwa safari za treni za abiria imetokana na ongezeko la abiria wanaosafiri kwa ajili ya msimu wa sikukuu za krismasi na mwaka mpya na vilevile kufungwa kwa shule na vyuo vingi msimu huu wa mwisho wa mwaka.

Akiongea wakati wa mahojiano Kaimu Mkurugenzi Idara ya Uendeshaji Bwana Focus Sahani amefafanua kuwa treni kutoka Dar Es Salaam kwenda Moshi na Arusha zitakuwa zikisafiri siku za Jumatatu , Jumatano na Alhamis na treni kutoka Arusha na Moshi kuja Dar Es Salaam zitakuwa zikisafiri siku za Jumanne na Alhamis.

Aidha Bwana Sahani ameongeza kuwa kuelekea sikukuu ya Krisimasi Desemba 25 , 2023 na ongezeko la abiria wanaosafiri mikoa ya kaskazini Shirika la Reli Tanzania limeongeza treni ya ziada ( special train ) ambayo itasafiri siku ya Jumamosi Disemba 23 , 2023 saa mbili (2) asubuhi kutoka Dar Es Salaam kwenda Moshi na Arusha.

Treni hiyo itakuwa na mabehewa 18 ambapo mabehewa tisa (9) yatakuwa ni ya daraja la tatu , mabehewa manne (4) yatakuwa daraja la pili kukaa na mabehewa manne (4) yatakuwa daraja la pili kulala.

"Shirika la Reli Tanzania tunawajali abiria wetu na Watanzania kwa ujumla ,tumeona kuna haja ya kuongeza treni maalum kwa ajili ya kuwapeleka watu Kula sikukuu Moshi na Arusha, Jumamosi asubuhi treni itaondoka hapa saa mbili kamili asubuhi ,treni hii ni maalumu " Amesema Bwana Sahani.

Bwana Stanley Msuya ambaye ni abiria wa treni amesema kuwa anaishukuru sana Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania kuendelea kuboresha usafiri wa treni kwani unawasaidia Watanzania wengi hasa ambao hawawezi kumudu ongezeko la bei ya mabasi msimu huu wa sikukuu kutokana na hali ya kiuchumi.

"Mimi ni mdau wa treni siku zote kwanza usafiri wa treni ni bei rahisi mnoo ukilinganisha na mabasi na ndege na pia hakuna usumbufu, ukipanda treni kila kitu unakipata ndani ya treni mpaka mwisho wa safari" amesema Stanley .

Kwa sasa bei za treni zinazofanya safari kutoka Dar es Salaam mpaka Moshi ni Shilingi 16500/= daraja la tatu, Shilingi 18100/= daraja la pili kukaa na Shilingi 39100/= daraja la pili kulala

Vilevile bei ya safari za treni kutoka Dar es Salaam hadi Arusha ni Shilingi 18,700/= daraja la tatu, Shilingi 23700/= daraja la pili kukaa na shilingi 44100/= daraja la pili kulala.