SHIRIKA LA RELI TANZANIA LAENDELEA NA ZOEZI LA ULIPAJI FIDIA ILI KUPISHA UJENZI WA NGUZO ZA UMEME WA SGR
November
2019
Shirika la Reli Tanzania laendelea na zoezi la ulipaji fidia ili kupisha ujenzi wa Miundombinu ya kusafirisha umeme katika mradi wa reli ya kisasa - SGR kipande cha Dar es Salaam - Morogoro, hivi karibuni Novemba, 2019.
Zoezi linaendeshwa na Maafisa kutoka Shirika la Reli Tanzania, Shiirika la Usambazaji Umeme nchini - TANESCO, Chuo Kikuu cha Ardhi na viongozi wa serikali za mitaa na vijiji husika katika kijiji cha Mtego wa Simba, Kinonko, Kidugalo, Mikese, Sinyaulimbe, Ngerengere, Mgude, Mhungamkola na mtaa wa Pangawe.
Malipo ya fidia yanahusisha wananchi wote ambao maeneo yao yamepitiwa na ujenzi wa miunbominu ya usafirishaji wa umeme kutoka katika chanzo cha uzalishaji kwenda katika vituo vya kuhifadhi na kupoza umeme ambavyo vitapeleka umeme katika treni za kisasa.
Aidha wananchi wa mitaa na vijiji hivyo wameonesha ushirikiano katika zoezi hili ambapo zaidi ya wananchi 200 watapatiwa hundi zao kwa ajili ya fidia za ardhi na makazi mkoani Morogoro. Mkazi wa kijiji cha Mtego wa Simba Bwana Rashid Said ambaye eneo lake limetwaliwa amesema kuwa manufaa ya mradi wa SGR ni makubwa kuliko fidia ambazo zimekuwa ziilipwa hivyo anaunga mkono jitihada za serikali.
Shirika linaendelea kuwaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za Mradi wa Ujenzi w Reli ya kisasa, kwani mradi huu ni wa kimkakati na wenye maslahi kwa taifa katika sekta za uchumi, utawala na jamii, pia linawashukuru wananchi wote wanaoshiriki kwa namna yoyote katika kuhakikisha mradi huu unaotumia fedha za watanzania haukwami.