Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​SHIRIKA LA RELI LAENDELEA NA KAMPENI YA ELIMU YA UELEWA KUHUSU USALAMA NA ULINZI WA MIUNDOMBINU YA RELI


news title here
15
August
2020

Katika muendelezo wa Kampeni ya Uelewa kuhusu namna ya kudhibiti ajali katika reli kwa kuzingatia alama za usalama katika miundombinu ya reli Shirika limeendelea na zoezi hilo kwa kufanya mikutano na wananchi wa vijiji vya Madala, Madumu na Chekelei katika kata ya Chekelei na katika vijiwe vya bodaboda wilayani Korogwe mkoani Tanga Agosti 15, 2020.

Mikutano hiyo iliongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mhe. Kissa Kasongwa akiwa na Katibu Tawala wilaya ya Korogwe Bi. Rahel Muhando na Afisa Tarafa ya Mombo Wilaya ya Korogwe Bwana Alex Mhando wakishirikiana na maafisa wa Shirika la Reli ambao wanaendelea na zoezi hilo wakitokea mkoani Arusha.

Aidha Mkuu wa Wilaya ya Korogwe amesema kuwa kila mtanzania anachangia katika sekta ya maendeleo kupitia kodi, hivyo maendeleo haya ya kuwepo kwa reli ni matokeo ya kodi hivyo wananchi wote wanapaswa kuithamini reli ili iweze kuwa salama muda wote, pia amewasisitiza wananchi wanaoishi karibu na reli kuchukua tahadhari wakati wote hususani kwa watoto wadogo wanaokatiza reli mara kwa mara.

“Kila mtanzania anachangia maendeleo ya nchi yake, sisi tukishaona thamani ya reli hii tutailinda pia nawaomba mchukue tahadhari katika kuwachunga watoto kucheza au kukatiza katika maeneo ya reli” alisema Mkuu wa Wilaya ya Korogwe

Baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano katika kijiji cha Chekelei wamesema kuwa wamelishukuru Shirika kwa kuwapatia elimu hiyo sambamba na kushukuru jitihada zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kurejesha usafiri huo ambao umekuwa na faida kubwa kwa wakazi wa eneo hilo.

“Namshukuru Rais Magufuli kwa kutuletea treni, inatusaidia sana” alisema Bi. Amina Pazi Shelukindo, Mkazi wa kijiji cha Chekelei

Timu ya Mawasiliano kutoka TRC imefanya Kampeni iliyodumu kwa majuma mawili kuhusu uelewa wa masuala ya ulinzi na usalama wa miundombinu ya reli kupitia vyombo vya habari na mikutano ya ana kwa ana na wananchi wa mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Arusha ili kuwapa utayari wananchi kupokea huduma za treni zilizorejeshwa hivi karibuni kati Dar es Salaam na Moshi na ile ya Dar es Salaam, Tanga – Moshi – Arusha ambayo inatarajiwa kurejeshwa hivi karibuni