Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​SGR KUWA CHACHU YA MAENDELEO VIJIJINI


news title here
21
May
2022

Shirika la Reli Tanzania - TRC linaendelea na zoezi la kutwaa ardhi katika maeneo mbalimbali kupisha mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa - SGR kipande cha tano Isaka - Mwanza linalofanyika wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza hivi karibuni Mei, 2022.

Vijiji vilivyopitiwa na mradi wa SGR katika wilaya hiyo ni pamoja na Nkalalo, Ligembe na kijiji cha Isunga ambapo maeneo kadhaa ya makaburi ya wapendwa wao yamehamishwa ikiwemo eneo litakalopita njia kuu ya reli ya SGR pamoja sehemu za kuchukua vifusi.

Afisa masuala ya kijamii kutoka TRC Bi. Joyce Ponela ameeleza kuwa wananchi wanapata fursa ya kupewa kazi za zoezi katika maeneo yao ili kuweza kujipatia kipato na pia kuendelea kunufaika na mradi.

“Tunatoa kipaumbele cha kuchukua vibarua katika eneo husika ili kumpa fursa kila mwananchi kujipatia kipato” alisema Bi. Joyce.

Aidha, Bi. Joyce alisema kuwa zoezi hilo linazingatia taratibu za kiafya pamoja na haki zote za kijamii pamoja na kuruhusu wananchi kufanya mila zao na maombi kabla ya zoezi kufanyika.

“Tuna imani tofauti hasa vijijini mambo ya mila bado yanaendelea hivyo tunawapatia nafasi wananchi kufanya mila zao” alisema Bi. Joyce.

Naye Afisa Tarafa katika tarafa ya Ibindo wilayani Kwimba Bw. James Chuwa alisema kuwa wananchi wanaendelea kupata uelewa wa kuwa na eneo maalumu la maziko katika vijiji ili kuweka mpangilio mzuri wa ardhi na makazi katika maeneo yao.

“Tunajitahidi kutoa elimu hasa katika mazoezi kama haya ili kuwafumbua macho wanakijiji waache mambo ya kizamani na kufuata nyakati kadri zinavyobadilika ili kuleta maendeleo katika maeneo yao” alisema Bw. Chuwa.

Mwananchi kutoka kijiji cha Ligembe Bw. Baraka Kiberiti ameipongeza TRC kupitia serikali ya awamu ya sita kwa kuendeleza miundombinu ya ujenzi wa reli ya kisasa pamoja na kutoa fursa za kazi kwa vijana katika maeneo yao na kuzidi kuhamasisha maendeleo vijijini.

“Mimi kama kijana nafurahi sana kupata fursa ya kufanya kazi katika mradi wa SGR, vijana ndio nguvu ya nchi yetu tukazane kufanya kazi kwa juhudi” alisema Bw. Kiberiti.

Zoezi hilo la kutwaa ardhi kupisha mradi wa SGR kipande cha tano Isaka - Mwanza ni zoezi endelevu ambapo hadi sasa hatua ya ujenzi katika kipande hicho kimefikia asilimia 5.74.

Tanzania Census 2022