SGR KUCHOCHEA UKUAJI WA UCHUMI NA BIASHARA TANZANIA NA BURUNDI

February
2025
Shirika la Reli Tanzania (TRC), linaendelea na ziara ya kukutana na wadau wa taasisi mbalimbali kutoka nchi za Tanzania na Burundi, kufuatia mradi wa ujenzi wa reli yenye kiwango cha kimataifa - SGR kwa awamu ya pili ya ujenzi katika kipande cha saba kutoka Uvinza - Malagasi na kipande cha nane kutoka Malagarasi - Msongati iliyoanza kufanyika hivi karibuni Februari, 2025.
TRC kwa pamoja na timu kutoka Burundi wanafanya ziara hiyo kwa lengo la kushirikisha wadau kutoka ngazi mbalimbal ikiwemo Mkuu wa mkoa wa Kigoma, Balozi mdogo wa Burundi pamoja na wakuu wa wilaya zilizomo mkoani humo, Vyombo vya ulinzi na usalama , wadau wa mazingira sambamba taasisi za serikali ambazo zitashiriki kwa karibu katika ujenzi wa mradi huo ikiwemo Wakala wa Barabara za Vijijini - TARURA, Wakala wa Barabara Tanzania - TANROADS, Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira- DAWASA, Shirika la Umeme Tanzania - TANESCO.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye alieleza kuwa mradi huo wa SGR ukikamilika kwa vipande vya Tabora - Kigoma, Uvinza - Malagarasi na Malagarasi - Msongati vinaweza kuwa chachu ya ukuaji wa uchumi kati ya nchi ya Tanzania na Burundi.
“Kigoma inaweza kugeuka kuwa kitovu cha uchumi na biashara kwenye ukanda huu wa Magharibi” alisema Mhe. Thobias Andengenye.
Aidha Mhe. Thobias Andengenye alisema kuwa anaipongeza TRC kwa kushirikisha viongozi na wananchi juu ya maswala ya mradi kabla na baada ya ujenzi kwani itasaidia katika kurahisisha ujenzi sababu ya kupewa elimu ya kutosha.
“Watu wanapaswa kujua kwamba SGR ni yao hii itasaidia katika swala la ulinzi na usalama ili wakiona mtu yeyote anaehujumu miundombinu ya SGR ni adui wa wote” aliongezea Mhe. Thobias Andengenye.
Aidha Katibu Mkuu wa Miundombinu kutoka nchini Burundi Mhe. Mhandisi Nijimbere Egide ameeleza kuwa kwa upande wa nchi ya Burundi watajifunza mambo mbalimbali ya kiutaalamu juu ya miundombinu ya ujenzi wa reli kupitia TRC pamoja na kuleta wataalamu kuja kupata mafunzo ya uhandisi na uendeshaji wa miundombinu ya SGR.
“ Tunashukuru sana kwa mapokezi mazuri na tunaimani tutafikia lengo lililokusudiwa hadi mradi huu utakapokamilika” alisema Mhe. Mhandisi Nijimbere Egide.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi wa Ujenzi na Miundombinu wa TRC Mhandisi Machibya Masanja, alisema kuwa awamu ya pili ya ujenzi imegawanyika katika vipande vitatu ambavyo ni kipande cha sita Tabora - Kigoma chenye urefu wa kilometa 506, kipande cha saba na cha nane kutoka Uvinza - Msongati chenye kilomita 240 na kipande cha tisa Kaliua - Mpanda Karema chenye kilometa 307.
“Kutokana na ujenzi huu kuna kambi zitakaa maeneo ya nchi ya Burundi na kambi nyingine zitakua ndani ya mpaka wa nchi ya Tanzania” alieleza Mhandisi Machibya Masanja.
Aidha Mhandisi Machibya aliwatolea wito wakala wa ujenzi wa barabara kuhakikisha wanaunganisha vituo vya reli na biashara ili kutowafanya wananchi kuuchukia mradi kwa kukosa njia za kuwafikisha kwa wepesi katika stesheni.
Ziara hiyo ya ushirikishwaji wadau mbalimbali inaendelea hadi nchini Burundi ambapo italeta uelewa wakutosha kwa viongozi ili kuweza kijipanga vema wakati wa kusanifu mradi huo wa ujenzi wa SGR kutoka Uvinza - Malagarasi na Malagarasi - Msongati.