Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

SERIKALI YAWAPA HAMASA WANAKIJIJI KINONKO KUFANYA MAENDELEO


news title here
30
August
2020

Serikali imetoa hamasa kubwa kwa wananchi katika kijiji cha Kinonko katika kujikita kufanya maendeleo baada ya zoezi la ulipaji wa fidia linalofanywa na Shirika la Reli Tanzania ili kupisha ujenzi wa reli ya kisasa - SGR kipande cha Dar es Salaam - Morogoro, Agosti 2020 hivi karibuni.

Hamasa hiyo ambayo imewapelekea wanakijiji kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo linaloendelea ili kuweza kupatiwa hundi zao na maafisa kutoka TRC.

Wananchi wote ambao maeneo yao yametwaliwa na mradi huo wa SGR wameahidi kuzitumia pesa hizo vizuri katika kuleta maendeleo ya kijiji kwa kufanya biashara mbalimbali pamoja na kujenga nyumba za kisasa.

Licha ya mikakati hiyo ya maendeleo, wamefurahishwa sana na ujio wa mradi wa reli ya kisasa na kusema kuwa mradi huo ukikamilika utawarahisishia usafiri kwa kutumia muda mfupi pamoja na urahisi wa ufanyaji wa biashara katika kijiji hicho.

Hata hivyo Mhasibu kutoka TRC Bw. Jovian Mtembei amesema kuwa wameambatana na maafisa wa Benki ya NBC ili kuwapa urahisi wanakijiji wasiokuwa na akaunti za benki kufungua na kuweka fedha zao.

“Tumerahisisha kwa kuja na huduma za kibenki kwa kuambatana na NBC ili kuepusha mambo mbalimbali yanayoweza kujitokeza ikiwemo upotevu na uharibifu wa hundi “ alisema Bw. Mtembei .

Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania inahakikisha kuwa watu wote ambao maeneo yao yametwaliwa na mradi huo wa SGR wanapatiwa malipo yao ili kuwapa urahisi wakandarasi kuendelea na ujenzi na kumaliza kwa wakati unaostahiki.

Vilevile kuwapatia wananchi haki zao stahiki na kuwaasa kuachia maeneo hayo kwa siku ambazo wameagizwa mara tuu baada ya malipo hayo.