Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​SERIKALI YAENDELEA KUUPIGA MWINGI SEKTA YA RELI NCHINI


news title here
22
March
2025

Tarehe 22 Machi 2025, Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania - TRC Ndugu Masanja Kungu Kadogosa amefanya mkutano na waandishi wa habari kwaajili ya kutoa taarifa ya mafanikio Serikali ya awamu ya sita kwenye sekta ya reli katika ukumbi wa mikutano wa habari maelezo jijini Dodoma.

Mkurugenzi Kadogosa amewaeleza waandishi wa habari kuwa, wakati Rais wa awamu ya sita anaingia madarakani aliahidi kumalizia ujenzi wa SGR Dar es Salaam - Morogoro na Morogoro - Makutupora ambapo alikuta ujenzi wa SGR Dar es Salaam - Morogoro upo asilimia 83.55 na Morogoro - Makutupora 57.57 na mnamo Juni 2024 vipande hivi vilikamilika na kuanza kutoa huduma ya usafirishaji wa abiria.

Shirika lilianza kutoa huduma ya usafirishaji wa abiria tarehe 14 Juni 2024 kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro na mnamo tarehe 25 Julai 2024 shirika liliongeza safari ya Dar es Salaam hadi Dodoma na tarehe 01 Agosti 2024 Mhe. Rais Dkt. Samia Hassan Suluhu Hassan alizindua rasmi uendeshaji wa treni za abiria kati ya Dar es Salaam hadi Dodoma.

"Hadi sasa takribani abiria milioni 2.1 wamesafiri na treni ya SGR na jumla ya shilingi bilioni 59 za kitanzania zimekusanywa kama mapato" amesema Kadogosa.

Aidha, ameongeza kua Serikali ya awamu ya sita ilianzisha ujenzi wa SGR katika vipande vipya vitatu kwaajili ya kukamilisha ujenzi wa reli ya SGR awamu ya kwanza Dar es salaam - Mwanza ambavyo ni Makutupora - Tabora 14.53%, Tabora - Isaka 6.61% na Isaka - Mwanza 63.10%. Pia serikali ya awamu ya sita ilianzisha utekelezaji wa ujenzi wa SGR awamu ya pili Tabora - Kigoma km 506 ambayo umefikia 7.81% pamoja na utekelezaji wa Uvinza - Malagarasi - Musongati ambapo ununuzi wa mkandarasi na msimamizi wa mradi ushakamilika na mkataba ulisainiwa tarehe 29, Januari 2025.

Shirika linategemea kuanza huduma ya usafirishaji wa mizigo mwezi Aprili 2025 kufuatia kukamilika kwa majaribio ya mabehewa 264 ya mizigo yaliyowasili nchini Disemba 2024 ambapo linatarajia kusafirisha mzigo mkubwa kwani treni moja itakua inabeba kiasi cha tani 3000 kwa wakati mmoja.

"Usafirishaji huu wa mzigo utapelekea kupungua kwa gharama za usafiri na hivyo kupungua kwa bei za bidhaa sokoni na itasaidia kupunguza gharama za matengenezo ya barabara kwani mizigo mikubwa itasafirishwa kwa njia ya reli, vilevile SGR itachangia ufanisi wa bandari na ukuaji wa sekta zingine ikiwemo nishati,kilimo na viwanda pamoja na ukuaji wa miji katika maeneo yaliyopo katika ushoroba wa reli" amesisitiza Kadogosa.

Kadhalika, Mkurugenzi Kadogosa ameongeza kuwa, Shirika limeendelea na utekelezaji wa ukarabati wa reli ya kati kwa awamu ya kwanza ambapo Dar es Salaam - Isaka umekamilika na linaendelea kutekeleza katika vipande vya Kaliua - Mpanda pamoja na ukarabati wa madaraja), Ujenzi wa daraja na mabadiliko ya njia kati ya Godegode - Gulwe, vilevile ununuzi wa reli, mataruma na vifungashio kwaajili ya ukarabati wa reli ya Isaka - Mwanza, Ruvu - Mruazi Junction pamoja na maandalizi ya utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi wa ukarabati wa reli ya kati (TIRP - 2).

Shirika la Reli limeendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kusimamia ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya reli ,utoaji huduma za usafirishaji wa abiria na mizigo nchini.