Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

FINAL RAP REPORT UVINZA KIGADYE


news title here
16
March
2025

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) ikiambatana na menejimenti ya Shirika La Reli Tanzania - TRC, Machi 15, 2025 imefanya ziara ya kutembelea ujenzi wa mradi wa reli ya kiwango cha kimataifa (SGR) kipande cha sita kutoka Tabora hadi Kigoma.

Kamati ya PIC chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Augustine Vuma, imeeleza kuwa serikali itaendelea kuwekeza fedha kwaajili ya ujenzi wa SGR katika vipande vyote vya awamu ya kwanza na awamu ya pili.

“Kwa sasa fedha zinazotumika kujengea mradi huu ni fedha za makusanyo ya serikali, naipongeza sana serikali kwa kuendeleza ujenzi wa SGR” aliongezea Mhe. Vuma.

Kamati hiyo ya PIC awaliilitembelea ujenzi wa daraja la reli katika eneo la mto Malagarasi na baadae kukagua kambi za wafanyakazi zilizopo wilayani Uvinza Mkoa wa Kigoma.

“Tumejiridhisha kuona maendeleo ya mradi kipande hiki cha sita na tumeona mradi upo asilimia saba (7%) za utekelezaji na tumeona daraja lililopo katika mto Malagarasi, kambi za wafanyakazi zimeshakamilika na kuna baadhi ya sehemu wameshachonga mtaro kwaajili ya tuta la reli” alieleza Mhe. Augustine Vuma.

Katika hatua nyingine Mhe. Vuma alisema kuwa wananchi kanda ya Magharibi pamoja na nchi jirani Congo na Burundi wanaisubiri reli ya SGR ili kuweza kusafirisha mizigo kiurahisi kwa gharama nafuu na uharaka zaidi ili kukuza uchumi wa mataifa ya Afrika Mashariki.

Wakati huohuo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TRC Bw. Ally Karavina alisema kuwa serikali imelenga kubadilisha uchumi wa wananchi na nchi kiujumla na ujenzi wa reli hiyo ya SGR utaleta faida kubwa zaidi pindi usafirishaji wa mizigo utakapoanza kufanyika.

“Tunajenga sehemu nyingi na tutakapokuja kumaliza tutamaliza kilometa zaidi ya elfu mbili kwa mara moja na reli yenye kiwango sawa vya ubora kwa vipande vyote” alisema Mwenyekiti huyo wa bodi wa wakurugenzi wa TRC.

Bw. Karavina aliongezea kubainisha kuwa usafirishaji wa mizigo kwa njia ya reli utasaidia bandari ya Dar es Salaam kupata mizigo ya kudumu wa kwenda nchi za nje na kuifanya bandari hiyo kuwa imara kuliko bandari zote za Afrika Mashariki.

Utekelezaji wa Ujenzi wa SGR kipande cha sita Tabora - Kigoma Unaendelea ambapo TRC inahakikisha ujenzi huo kuwa ni wenye kiwango sawa na vipande ambavyo ujenzi umekamilika na shughuli za uendeshaji zimekwisha anza kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma.