Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​SAFARI ZA TRENI ZA ABIRIA KATI YA DAR ES SALAAM NA ARUSHA ZAREJEA RASMI


news title here
03
October
2020

Treni ya kwanza ya abiria wasili katika Stesheni ya Arusha jijini humo baada ya zaidi ya miaka 30 na kupokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe. Kenani Kihongosi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha pamoja na maelfu ya wakazi wa jijini humo Oktoba 03, 2020.

Treni hiyo ya abiria iliruhusiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Abubakar Kunenge katika Stesheni ya Kamata Dar es Salaam kuelekea Oktoba 02, 2020.

Mkuu wa Wilaya ya Arusha kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha amesema kuwa wamefurahishwa na ujio wa treni hiyo kwani unakwenda kufungua fursa za ajira na biashara kwa wakazi wa jiji hilo

“Sisi kama wananchi wa jiji wa Arusha tunafarijika sana na ujio wa treni hii, kwa sababu inakwenda kufungua fursa za uchumi kwa jiji letu la Arusha kwa sababu vijana watakwenda kupata ajira na biashara zinakwenda kufanyika” alisema Kihongosi

Mhe. Kenani ameongeza kuwa unafuu wa nauli katika usafiri wa treni una faida kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa Arusha na nchi kwa ujumla “Kama kwenye basi mtu anaweza kulipa Shilingi 32,000 kwenye treni akalipa 16,000 anaweza kuokoa kiasi cha fedha ambacho kinaweza kusaidia kufanya mambo mengine, kwahiyo hii ni fursa kubwa tunamshukuru na kumuombea sana Mhe. Magufuli” aliongeza

Halikadhalika, Mhe. Kihongosi amewasisitiza wananchi wa jiji la Arusha kuendelea kuitunza reli ili iweze kuleta manufaa kwa watanzania wote kwa ujumla na kuwataka wananchi kumuunga mkono Rais Magufuli kwa jitihada anazozifanya katika kuboresha sekta ya miundombinu ya reli nchini.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TRC Prof. John Wajanga Kondoro amemshukuru Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa maamuzi yake ya kuwekeza katika uboreshaji wa sekta ya miundombinu ya reli nchini, pia ameahidi kuendelea kusimamia utekelezaji wa maagizo ya Mheshimiwa Rais katika kuboresha sekta ya usafiri wa reli nchini.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Ndugu Masanja Kungu Kadogosa ameeleza kuwa usafiri wa reli katika mikoa ya Kaskazini umerejea na utaendelea kuwepo kwani Shirika limeandaa mikakati ya kuboresha huduma ya usafiri katika maeneo hayo kwa kuanzisha huduma ya usafiri wa treni za mjini kati ya Moshi na Arusha ambayo inatarajiwa kuanza hivi karibuni lakini pia kwa kujenga reli mpya ya viwango vya kimataifa - SGR kuanzia Tanga – Moshi – Arusha hadi Musoma.

Baadhi ya wananchi waliohudhuria sherehe hiyo wameeleza furaha yao kwa kurejea kwa treni za abiria huku muitiko ukiwa mkubwa zaidi kwa wananchi kutumia huduma hiyo ambapo wananchi wengi walionekana wakiendelea kununua tiketi kwa ajili ya safari kuelekea jijini Dar es Salaam.

“Kwa kweli siamini hiki ninachokiona, namshukuuru Rais Magufuli nawashukuru TRC wamefanya kazi kubwa kurejesha huduma hii iliyosimama kwa muda mrefu, sasa tutapata fursa za kufanya biashara na shughuli nyingine za kiuchumi” alisema Zubeda Ally, mkazi wa Arusha.

Treni ya abiria ya Deluxe inafanya safari kati ya Dar es Salaam na Arusha siku za Ijumaa na Jumatatu kutoka Dar es Salaam na Jumamosi na Jumanne kutoka jijini Arusha ambapo kwa mwezi Oktoba Shirika limetoa ofa ya punguzo la asilimia 15 kwa nauli za treni kwa madaraja yote.