RELI YA SGR KUKUZA UCHUMI WA AFRIKA
May
2024
Tume ya Umoja wa Afrika chini ya Idara ya miundombinu na nishati wametembelea mradi wa kimkakati wa reli ya kiwango cha kimataifa - SGR kipande cha kwanza Dar es Salaam - Morogoro Mei 10, 2024.
Lengo la ziara ni kuona maendeleo ya ujenzi pamoja na mpango mkakati wa uendeshaji wa reli ya kisasa pindi itakapoanza usafirishaji.
Mkuu wa idara ya usafirishaji, miundombinu na nishati wa Tume ya Umoja wa Afrika Mhandisi Eric Ntagengerwa amesema kua katika umoja wa Afrika usafiri wa reli una jukumu kubwa na kupitia kasi kubwa ya usafiri wa SGR itarahisisha usafirishaji wa bidhaa na mizigo ambayo itasafirishwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
"Tanzania imefanya mengi na tunajua baadhi ya sehemu zitaanza uendeshaji na zingine zitatarajiwa kuanza hivi karibuni, kupitia safari hii tumepata uzoefu mkubwa sana kutoka Tanzania kwenye sekta ya reli na bandari" amesisitiza Mhandisi Eric.
Mkurungenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania - TRC Ndugu Masanja Kadogosa amesema uwekezaji wa reli ya SGR umelenga kujenga na kuimarisha muingiliano wa nchi za Afrika ili kufanya biashara na kukuza uchumi katika nchi za Afrika.
"Afrika imejiwekea lengo hadi kufikia mwaka 2060 iwe imeunganishwa na mtandao wa reli na ukiangalia Tanzania hadi sasa tupo kwenye kilomita 5000 inakaribia 7000" ameongeza Kadogosa.
Mhandisi Achieng' Akon kutoka Umoja wa Afrika Mashariki ameipongeza Tanzania kwa kuweza kusimamia na kuweza kufanikisha ujenzi wa reli ya SGR, tunatarajia kuona uwekezaji kwa maendeleo ya reli ya SGR katika sekta ya usafirishaji.
Mkurungenzi wa Miundombinu wa Umoja wa Afrika Mashariki Mhandisi Godfrey Enzama ameipongeza Tanzania kwa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa kulingana na mpango mkakati wa reli ya Afrika Mashariki wa mwaka 2010 na kupitia utelekelezaji wa reli hii utaleta chachu katika kuinua uchumi kwenye ushoroba wa kati na ushoroba wa Kaskazini.
"Tunaangazia reli hii kusaidia maendeleo ya kiuchumi hasa katika shoroba kuu za kiuchumi za kati na Kaskazini ambazo ni muhimu kwa nchi zisizo na pwani katika eneo hilo"amesisitiza Mhandisi Enzama
Ujenzi wa mradi wa reli ya reli ya kisasa SGR kipande cha kwanza Dar es Salaam - Morogoro hadi Sasa umefikia asilimia 98.96% na mkandarasi amebakiza hatua chache za mwisho za kumalizia ujenzi.