Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​RAIS MAGUFULI ALIPONGEZA SHIRIKA LA RELI KWA USIMAMIZI MZURI WA MRADI WA SGR


news title here
28
June
2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amelipongeza Shirika la Reli Tanzania – TRC kwa usimamizi mzuri wa ¬Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa – SGR baada ya kuridhishwa na kasi ya maendeleo ya mradi huo kipande cha Dar es Salaam – Morogoro, Juni 28, 2020.

Rais Magufuli ameanza ziara ya siku mbili kuanzia Dar es Salaam hadi Kilosa mkoani Morogoro kwa lengo la kukagua Mradi wa SGR unaotekelezwa kuanzia Dar es Salaam hadi Makutupora mkoani Singida ambapo ujenzi wake umefika zaidi ya 82% kwa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro na 38% kwa kipande cha Morogoro – Makutupora.

Katika ziara yake Mhe. Rais aliongozana na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Isack Kamwelwe, Mkuu wa Jeshi la Polisi Simon Sirro, Mkuu wa mkoa wa Pwani Eng. Everest Ndikilo, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Asunta Mshana, viongozi wa Chama cha Mapinduzi – CCM na uongozi wa Shirika la Reli Tanzania ukiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Prof. John Wajanga Kondoro na Mkurugenzi Mkuu wa TRC Ndugu Masanja Kadogosa.

Aidha, Mheshimiwa Rais amesema kuwa ameridhishwa na maendeleo ya mradi na amewapongeza wakandarasi kwa kazi nzuri wanayofanya

“Wakandarasi mnafanya kazi nzuri, nimeona kazi za ‘Structure’ kule na nina uhakika mpaka kwenda huko mbele wamefanya kazi nzuri, nataka nihakikishe wanamaliza mapema, wananchi wa Soga na wananchi wote watumie usafiri huu kwa sababu ni muhimu katika maisha yao” alisema Mhe. Rais

Rais Magufuli amesema kuwa mradi wa SGR unatumia fedha nyingi ambazo ni mapato ya ndani hivyo kuna haja ya kuhakikisha wananchi wanaoishi katika maeneo ya mradi wananufaika na mradi huo kwa kupata huduma za afya, maji, elimu na fursa za biashara katika maeneo ambayo mradi huo umepita hususani Stesheni mpya zinazojengwa “Mradi huu unagharimu fedha nyingi, ni zaidi ya Trilioni 7 na fedha zote hizi zimetolewa na watanzania, ninataka hapa pawe pazuri, na hawa wananchi wenye uwezo wa kufanya biashara wafanye ili wafaidike na hii treni” alisema Mhe. Magufuli

Rais Magufuli katika kuhakikisha wananchi wa Soga wananufaika na mradi huo mkubwa amemtaka Waziri wa Ujenzi na Mkurugenzi wa TRC kuhakikisha wanajenga kituo cha afya ili wananchi wapate huduma ya matibabu, na huduma ya maji, pia aliendesha harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule ambapo Shirika la Reli Tanzania lilishikiri na jumla ya fedha Shilingi 68,500,000 zilipatikana.

Mhe. Rais amewaomba wananchi wa Soga mkoani Pwani kuendelea kutoa ushirikiano katika kulinda miundombinu ya reli na mradi huo ili kuhakikisha mradi huo unaisha kwa wakati kwa ajili ya manufaa yao na taifa kwa ujumla