Prof. MBARAWA AKAGUA UJENZI WA SGR KIPANDE CHA MWANZA - ISAKA

February
2025
Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa Februari 20, 2025, ametembelea na kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Reli ya kiwango cha kimataifa SGR, kipande cha Mwanza – Isaka katika eneo la Malampaka Mkoani simiyu.
Katika ziara hiyo Waziri Mbarawa aliambatana na Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Bw. Masanja Kadogosa, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Kenani Kihongosi na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Ndug. Shemsa Mohamed Seif.
Prof. Mbarawa ameeleza kuridhishwa kwake na kazi iliyofanywa na Mkandarasi ambapo kazi muhimu ya ujenzi wa tuta imefikia zaidi ya 89%.
Akitoa taarifa ya utekelezaji ya kipande hicho katika eneo la ujenzi wa stesheni ya Malampaka, Mkurugenzi mkuu wa TRC, Bw. Masanja Kadogosa, alisema kuwa ujenzi katika kipande hicho unaendelea vizuri ambapo kazi za utandikaji wa reli, ujenzi wa stesheni na usimikaji wa nguzo za Umeme zinaendelea.
“Mpaka sasa ujenzi umefikia 63.04% licha ya kusimama kidogo kwa sababu ya mvua, tunajipanga kuanzia mwezi Aprili, kuendeleza kazi kwa nguvu zaidi” alisema Kadogosa.
Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa ameitaka TRC kuzingatia changamoto zilizotokea katika vipande vya Dar Es Salaam hadi Dodoma, ili zisijirudie katika vipande vinavyoendelea na ujenzi, kikiwemo kipande cha Mwanza – Isaka.
“Jambo muhimu ambalo nataka wataalamu mlizingatie, kuna mambo tumejifunza kupitia uendeshaji katka vipande vya Dar Es salaam, Morogoro hadi Dodoma, lazima tuhakikishe kuwa hatuyarudii tena hapa, mfano ni ukubwa wa maeneo ya maegesho ya magari”
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Kenani Kihongosi, alielezea ujenzi wa reli kwa kipande cha Mwanza hadi Isaka namna ambayo umekuwa na manufaa makubwa kwa Wanasimiyu kupitia fursa mbalimbali zikiwemo ajira ambapo vijana 38 wamepata ajira kwenye mradi huo.
Ujenzi wa reli ya Kiwango cha kimataifa SGR kipande cha Mwanza – Isaka kina jumla ya KM 341 huku ujenzi wake ukigharimu zaidi ya Shilingi Trilioni 3 za kitanzania.