Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

MTANDAO MREFU WA RELI YA SGR KUCHOCHEA MAENDELEO YA KIKANDA NA AFRIKA -NCHEMBA


news title here
16
November
2026

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba amesema ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) ni uwekezaji wa kimkakati unaolenga kuleta mapinduzi katika sekta ya usafiri, kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.

Dkt.Mwigulu amesema kukamilika kwa mtandao wa SGR kutaiwezesha Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye mitandao mikubwa ya reli za kisasa duniani hatua itakayoongeza uwezo wa nchi katika usafirishaji wa abiria na mizigo na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika biashara ya kikanda na kimataifa.

Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati akifungua Mkutano wa 19 wa Tathmini ya Pamoja ya Sekta ya Uchukuzi (JTSR) unaofanyika katika Hoteli ya Malaika jijini Mwanza kuanzia Novemba 16 hadi 18, 2026.

Ameeleza kuwa uwekezaji katika sekta ya reli una manufaa makubwa kwa taifa ikiwemo kupunguza muda na gharama za usafirishaji, kuongeza ufanisi wa biashara, kufungua fursa za ajira na uwekezaji pamoja na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa kutoka maeneo ya uzalishaji kwenda katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Aidha, amesema maendeleo ya sekta ya reli yanachochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika maeneo mbalimbali nchini, kuongeza thamani ya maeneo yanayopitiwa na reli na kuboresha upatikanaji wa huduma na fursa za maendeleo kwa wananchi.

Kwa namna nyingine Waziri Mkuu amesisitiza umuhimu wa kuzingatia ubora, usalama na viwango vinavyotakiwa katika ujenzi na uendeshaji wa miundombinu ya reli ili kuhakikisha uwekezaji huo unaleta manufaa endelevu kwa taifa na vizazi vijavyo.

Akitoa salama za shukrani Kwa niaba ya Wizara ya Uchukuzi Waziri wa Uchukuzi Mhe.Prof.Makame Mbarawa amesema Wizara ya Uchukuzi itaendelea kusimamia ujenzi na maendeleo mbalimbali ya sekta ya Uchukuzi ikiwemo Reli ili kuimarisha shughuli za usafirashaji katika kukuza uchumi wa nchi na wananchi.

Ikumbukwe kuwa shirika la Reli Tanzania linaendelea na ujenzi, maboresho na ununuzi wa vifaa mbalimbali katika kuhakikisha sekta ya reli inakuwa chachu katika maendeleo ya nchi.