Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

MSEMAJI MKUU WA SERIKALI AFURAHISHWA NA MAANDALIZ YA TRC KUELEKEA KUANZA KUTOA HUDUMA KUTUMIA TRENI ZA SGR


news title here
04
January
2024

Msemaji Mkuu wa Serikali ambae pia ni Mkurugenzi Idara ya Habari Maelezo Bwana Mobhare Matinyi ametembelea ujenzi wa Reli ya Kimataifa SGR kipande cha kwanza Dar Es Salaam - Morogoro katika stesheni ya Dar Es Salaam, January 03, 2024.

Lengo la ziara hiyo nikujionea maendeleo ya ujenzi wa Reli ya SGR pamoja na kufahamu maandalizi na mikakati ya TRC kuelekea kuanza shughuli za uendeshaji hivi karibuni.

Baadhi ya masuala alioweza kufahamu Msemaji Mkuu wa Serikali ni pamoja na maendeleo ya ujenzi wa mradi wa SGR kuanzia kipande cha kwanza hadi cha tano ,ununuzi wa vifaa vya uendeshaji wa SGR ikiwemo mabehewa ,vichwa na vifaa vya matengezo , maandalizi ya wataalamu watakao hudumia treni ya SGR , upatikanaji wa umeme utakao tumika katika uendeshaji wa treni na mwisho suala la ulinzi wa miundombinu ya Reli na abiria.

Akiongea wakati wa ziara hiyo Bwana Matinyi ameeleza kufurahishwa kwake na TRC kwa kuweza kusimamia vyema ujenzi wa Reli yenye ubora na viwango vya Kimataifa ambavyo vitakidhi haja ya Watanzania.

" Watanzania wajiandae kupata huduma ya uhakika na ubora kwani Reli ya SGR ina viwango vya hali ya juu Kuanzia kwenye miundombinu ya Reli, vifaa vya uendeshaji na mifumo ya Usalama na ulinzi katika Reli hiyo " Amesema Bwana Matinyi.

Aidha ,Msemaji Mkuu amewataka wananchi kufahamu kuwa vifaa vinavoendelea kuwasili nchini ikiwemo mabehewa na vichwa ni lazima vifanyiwe majaribio( testing and Commissioning) ili kuhakisha Usalama katika kutoa huduma .

"La msingi Watanzania wanatakiwa kufahamu ujenzi wa Reli ya SGR unatumia utaalamu wa kisasa,kwa hiyo vichwa na mabehewa yanapo wasili nchini yanahitaji kupata muda wa majaribio ili kuhakikisha Usalama wa kusafirisha abiria ,ambapo kila kichwa kinahitaji kifikishe mwendo wa kilomita elfu kumi (10000) na kila behewa angalau lifikishe kilomita elfu 5000 katika majaribio hayo " Amesema Bwana Mobhare.

Nae Kaimu Mkurugenzi Mkuu Shirika la Reli Tanzania Mhandisi Machibya Masanja amesema kuwa TRC inaendelea na maandalizi mbalimbali kuelekea kuanza shughuli za uendeshaji ikiwemo majaribio ya vichwa na mabehewa yaliowasili nchini pamoja na wafanyakazi watakao hudumia katika treni za SGR.

"Kauli ya Mheshimiwa Raisi kwa ajili ya kuanza Uendeshaji inatuhamasisha kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha tunakamilisha baadhi ya vitu,

Kwa vichwa na mabehewa ambayo tumeyapokea tuko katika hatua mbalimbali za majaribio ,kwa sasa tunajaribu mifumo ya umeme ,brake ,injini na viyoyozi ili kuhakikisha ufanisi wake" Alisema Mhandisi Machibya.

Shirika la Reli Tanzania lipo katika maandalizi mbalimbali kuelekea kuanza shughuli za uendeshaji huku vifaa mbalimbali ikiwemo mabehewa na vichwa vya treni vikiendelea kuwasili kwa ajili ya Uendeshaji.