MRADI WA UBORESHAJI WA RELI YA KATI – TIRP DAR ES SALAAM - ISAKA WAFIKA 85%

June
2020
Mradi wa Uboreshaji wa Reli ya Kati – TIRP unaogharimu Dola za Kimarekani Milioni 300 upo mbioni kukamilika baada ya mradi huo kufika 85% baada ya kazi kubwa iliyofanyika kati ya Dar es Salaam – Isaka umbali wa Kilometa 970 tangu ulipoanza rasmi utekelezaji wake mwezi Juni 2018.
Mradi umelenga kufanya ukarabati wa Reli iliyopo kwa kipande cha Dar es salaam - Isaka ili kuongeza uwezo wa kubeba mzigo toka chini ya Tani 13.5 za uzito wa ekseli hadi tani 18.5 kwa kutandika upya njia za Reli Kilometa 312, kukarabati njia ya reli Kilometa 658, kukarabati makaravati na madaraja 44, kuboresha mfumo wa mawasiliano, kukarabati vituo vya kupakia na kupakua mizigo vya bandari ya Dar es salaam, Ilala na Bandari kavu ya Isaka pamoja na kununua mitambo ya ukarabati wa njia, vichwa vitatu vya treni na Behewa mpya 44 za mizigo, na kukarabati vichwa viwili vya treni.
Mratibu wa mradi wa TIRP Mhandisi Mlemba Singo ameeleza kuwa kwa ujumla maendeleo ya kazi yamefikia 85% huku kazi kubwa inayoendelea kwa kipande cha Dar es Salaam – Kilosa ni kubadilisha Reli na Mataruma kwa kuondoa ya zamani na kuweka mapya pamoja na kuboresha tuta la reli ili viweze kuruhusu kubeba uzito na kwenda mwendokasi iliyopangwa.
Pia ameongeza kuwa kipande cha Dar es Salaam - Kilosa wako katika hatua za mwisho ambapo takribani Kilometa 50 kati ya Kilometa 289 ndizo zilizobaki katika kuboresha njia hiyo ya reli na kipande cha kutoka Kilosa hadi Isaka kazi zilizobaki ni chache zikiwemo uwekaji alama za reli, ujenzi wa mitaro na kuhakiki viwango vitakavyoiwezesha treni kwenda mwendokasi wa Kilometa 70 kwa saa.
“Kazi hii kwa ujumla itaisha mwezi wa Kumi mwaka huu lakini itaisha kwa vipande, kipande cha kutoka Dar es Salaam hadi Kilosa kazi itaisha mwezi wa kumi lakini kipande cha Kilosa – Isaka kazi itaisha mwezi wa saba” alisema Singo
Mhandisi Singo aliongeza kuwa “Tumeshanunua Behewa 44 za mizigo ziko tayari kwa ajili ya kazi hii, vichwa vinatengenezwa pamoja na kuboresha mfumo wa mawasiliano ambao utawezesha kufungwa Kompyuta katika Stesheni na kuongoza treni kwa kutumia Kompyuta”
Naye Msimamizi wa Mradi wa TIRP kipande cha Dar es Salaam – Kilosa Mhandisi Christopher Calist amesema kuwa kazi kubwa inayoendelea katika kipande hiko ni kubadilisha Mataruma ya reli urefu wa Kilometa 20 zilizobaki, huku kazi ya kubadilisha sehemu ambazo reli imezeeka kuanzia Pugu mpaka Soga urefu wa Kilometa 14 na ujenzi wa Madaraja ikiwa imekamilika
Aidha, kutokana na janga la ugonjwa wa Corona wahandisi wanaendelea na kazi katika maeneo ya ujenzi kwa kuzingatia tahadhari na maelekezo yanayotolewa na Wizara ya Afya nchini ili kuhakikisha afya za wafanyakazi zinakuwa kipaumbele.
Bi. Jesca Bakari ambaye ni Mtaalamu wa Afya anaeleza kuwa “Tunahakikisha wafanyakazi kabla hawajafika maeneo ya kazi tunawaandalia vifaa ambavyo vitawakinga na ugonjwa wa Corona, tuna sabuni, vitakasa mikono pamoja na maji, tunawapatia Barakoa na Glavu pia tunawapatia elimu juu ya kujikinga na Corona”
Kukamilika kwa Mradi huu kutaboresha na kuongeza kiwango cha ubebaji mizigo kwa njia ya reli na madaraja, kuongezeka kwa mwendokasi wa treni toka Kilometa 30 hadi 70 kwa Saa na hivyo kupunguza gharama za usafirishaji,b kupunguza muda wa kupakia na kupakua mizigo kutoka Bandari ya Dar es salaam hadi bandari kavu ya Isaka kufikia Saa 24.
Maendeleo haya ya mradi inaonesha dhahiri jinsi serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mh.Rais Dk.John Pombe Magufuli ilivyodhamiria kuimarisha sekta ya miundombinu ya reli nchini na kuchochea Tanzania kuingia katika uchumi wa kati kwa haraka ifikakapo mwaka 2025.