Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​MRADI WA SGR KUWA CHANZO CHA UKUAJI WA UCHUMI MKOANI TABORA


news title here
23
March
2025

Serikali Wilaya ya Tabora Mjini, imempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuuendeleza mradi wa SGR kipande cha sita Tabora - Kigoma.

Pongezi hizo zimetolewa hivi karibuni na Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mjini Mhe. Deusdedith Katwale, wakati wa kampeni za uelewa wa mradi wa SGR kwa wananchi wa mkoa Tabora zinazofanywa na Shirika la Reli Tanzania (TRC).

Kampeni hizo za uelewa kwa jamii zina lengo la kuelimisha wananchi ambao wamepitiwa na mradi wa SGR masuala mbalimbali ikiwemo utwaaji wa ardhi kwenye maeneo ambayo mradi utapita, fursa za ajira, ushirikishwaji wa jamii husika, ulinzi na usalama kwenye miundombinu ya reli, usalama wa mali, raia na haki za binadamu.

Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mjini Mhe. Deusdedith Katwale, amewaasa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kuwa tayari kutoa maeneo yao pamoja na kuhudhuria vikao na kampeni zinazofanywa na TRC kwa faida ya jamii na nchi kiujumla.

“Miradi mikubwa ikipita katika Mkoa ni chanzo kikubwa cha kukuza uchumi kwani huduma za kijamii zinaongezeka ikiwemo ujenzi wa hospitali, shule, vyanzo vya maji, barabara hivyo vyote ni faida kwa wananchi” alifafanua Mhe. Katwale.

Wakati huohuo Mhandisi wa Mradi kipande hicho Benard Mero, alisema kuwa jumla ya kilometa 506 zitajengwa kwa njia kuu pamoja na njia za mapishano ambapo kati ya hizo kilometa 411 ni kwaajili ya njia kuu, pia kutakua na ujenzi wa kambi saba (7) za wahandisi na mkandarasi kati ya hizo kambi nne (4) tayari zimekamilika na kambi tano (5) zitajengwa za mhandisi mshauri na TRC kati ya hizo kambi moja (1) imeshakamilika.

“Shughuli zinazoendelea mpaka sasa ni ujenzi wa njia za mchepuko kilometa 50 kuanzia Usoke hadi Kaliua ndani ya wilaya Urambo na Kaliua, ardhi ilitwaliwa na wananchi wamelipwa fidia zao” alisema Mhandisi Benard Mero.

Aidha Mhandisi Mero alizungumzia ujenzi wa daraja la reli ya SGR kuvuka mto Malagalasi lenye mita 433.5 ambapo hadi sasa limekamilika kwa wastani wa asilimia 52% pamoja na shughuli za uchimbaji wa vifusi vya udongo na mchanga na upasuaji wa kokoto.

“Tunatarajia kupita katika mitaa mitano katika manispaa ya Tabora ambayo imepitiwa na mradi wa SGR ikiwemo mtaa wa Ipuli, Masagala, Izimbili, Ulamba, Tumbi na Isule Jeshini” aliongezea Mhandisi Benard Mero.

Katika hatua nyingine Afisa Tarafa Manispaa ya Mkoa wa Tabora Bw. Josephat Brown aliwaeleza wananchi kuwa wana wajibu wa kulinda miundombinu ya reli na kutoacha kuhudhuria kampeni za uelewa kwa jamii ili kujua taratibu na sheria zitakazoidhinishwa ili kuepusha malalamiko wakati kazi za ujenzi wa mradi zikiendelea.

Kampeni hiyo ya uelewa na uhamasishaji kwa wananchi ni endelevu katika kipande cha Tabora - Kigoma ili kuendelea kuwaelimisha wananchi katika nyanja tofauti kujua haki , taratibu na sheria pamoja na ulinzi na usalama kwa manufaa ya wananchi na nchi.