Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​MKUU WA WILAYA YA ARUMERU,TRC ANA KWA ANA NA WANAMERU KUENDELEZA KAMPENI YA UELEWA KUEPUSHA AJALI NA ULINZI WA RELI.


news title here
12
August
2020

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mh. Jerry Muro ameambatana na Viongozi kutoka Shirika la Reli Tanzania – TRC kuendeleza kampeni ya uelewa kuhusu ulinzi na usalama wa miundombinu ya reli inayoendelea katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Arusha Agosti 2020.

Lengo la Kampeni hii ni kutoa uelewa kwa wananchi kupitia vyombo vya habari na mikutano ya ana kwa ana katika makazi ya watu, vijiwe vya madereva, shuleni na katika vituo vya mabasi ili kuepusha ajali relini zinazoweza kupelekea vifo, uharibifu wa mali na miundombinu ya reli.

Katika muendelezo wa kampeni hiyo Shirika limeendelea na kampeni hiyo mkoani Moshi na jijini Arusha ambapo timu ya mawasiliano kutoka Shirika la Reli iliyopo mkoani Kilimanjaro imezunguka katika maeneo tofauti mkoani humo ikiwemo Wilaya ya Arumeru kwa vijiji mbalimbali na kwa upande wa Moshi kampeni imeendelea katika mtaa wa Bombambuzi, Fonga na Vijiji vya Rundugai, Mlima wa Shabaha, Sanya Stesheni, Mijongweni, Shirimgongani na kwa Tito pamoja na Shule ya Msingi Sanya Stesheni, Azimio na Weruweru.

Katika ziara hizo timu ya mawasiliano inashirikiana na viongozi wa maeneo husika kuanzia ngazi ya Kata, Tarafa, Vijiji na Vitongoji katika utoaji wa elimu hiyo kwa wananchi, pia Shirika linatumia fursa hiyo kukusanya maombi kutoka kwa wananchi kuhusu maeneo ya kuweka vivuko na Stesheni ndogo kwa ajili ya kushusha na kupakia abiria na mizigo kutokana na kwamba tangu reli hiyo iache kutoa huduma wananchi wameongezeka na kuanzisha vijiji katika maeneo ambayo hayakuwa na makazi hapo awali.

Aidha wananchi wengi wameonesha kufurahishwa na hatua hiyo iliyochukuliwa na Shirika la Reli Tanzania ya kutoa elimu ya uelewa kuhusiana na masuala ya ulinzi na usalama wa reli kwa wananchi wanaoishi maeneo ya kandokando ya reli kabla ya kuanza uendeshaji kwa kipande cha Moshi - Arusha, wananchi hao wameahidi kuhakikisha miundombinu hiyo inakuwa salama muda wote.

“Reli hii itasaidia wananchi wengi wa maeneo yanayozunguka reli hapa Kilimanajro, tutaweza kusafirisha mizigo lakini pia sisi wenyewe tutaweza kusafiri kuelekea Moshi na Arusha kwa urahisi zaidi” alisema Mohamed Saleh, Mkazi wa kijiji cha Shirimgongani

Halikadhalika viongozi na walimu wa Shule katika Mitaa na Vitongoji ambavyo timu hiyo ya mawasiliano imepita wameonesha ushirikiano na kuahidi kutoa ushirikiano katika kuelimisha jamii kuhusu ulinzi na usalama wa miundombinu ya reli kwani huduma za treni zitakapoanza kati ya Moshi na Arusha zitaleta fursa za ajira, biashara, uwekezaji na kuongeza hitaji la bidhaa za kilimo na ufugaji kutokana na kuwepo kwa usafiri nafuu na wa uhakika.