MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM ARUHUSU TRENI KWANZA YA ABIRIA DAR ES SALAAM KUELEKEA ARUSHA

October
2020
Shirika la Reli Tanzania - TRC limeanza kutoa huduma ya usafiri wa treni za abiria iliyokuwa imesimama kwa zaidi ya miaka 30 kati ya Dar es Salaam na Arusha, safari hiyo imeanza rasmi katika stesheni ya Kamata jijini Dar es Salaam hivi Oktoba 02, 2020.
Aidha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Abubakar Mussa Kunenge amepeperusha bendera kuruhusu treni kuanza huduma za usafirishaji mara baada ya shirika kujiridhisha kwa kufanya majaribio ya treni kutoka Dar es Salaam mpaka Arusha mwezi Agosti 2020.
Mkuu wa Mkoa alipata wasaa wa kuongea na abiria pamoja na wananchi ambapo alianza kwa kutoa pongezi kwa Serikali na Shirika kwa juhudi walizofanya kuhakikisha huduma ya usafiri wa reli inarejeshwa Arusha baada ya miaka zaidi ya 30 kusimama kutoa huduma.
“Niwapongeze Shirika na watendaji wote kwa kazi nzuri mliyofanya, kukosekana kwa huduma hii ilikuwa adha kwa wananchi wa kawaida, kwa sasa treni hii itakuwa ni mkombozi kwa wafanyabiashara., nwapongeze sana kwa kufahamu kwamba hamfanyi biashara kupitia wananchi wa kipato cha chini bali mnatoa huduma ndio sababu mmeweza kupunguza bei hiyo ni faraja kwetu sote” Mkuu wa Mkoa alisema.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Ndugu Masanja Kungu Kadogosa amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kujumuika katika tukio la kihisitoria ambapo amezungumzia jinsi alivyo na matumaini kwa wananchi wa Arusha watakavyoipokea treni hiyo kwa furaha na amewahakikishia wananchi kutoa huduma bora na salama kwa punguzo la bei 15% kwa mwezi Oktoba, huku akiwahakikishia kuwa treni hii haitakuja kupotea kama miaka 30 iliyopita.
Ndugu Kadogosa, alieleza namna usafiri wa reli ulivyo wa bei nafuu huku akitoa takwimu za bei usafirishaji wa Mbolea kwa mikoa ya kaskazini, “tunapeleka mizigo ukiangalia upande wa Mbolea kabla ya relii kuanza kazi walikuwa wanatumia usafiri wa kawaida ambapo walisafirisha Tani 1 kati ya Tsh 93,334 mpaka 100,000 lakini sisi tunasafirisha tani 1 kwa Tsh 46,000” Kadogosa alisema.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mkuu alielezea namna Shirika lilivyojipanga kwa sasa na baadae kuhakikisha usafiri wa reli ya kisasa – SGR unafika katika mikoa ya Kaskazini “hivi sasa tuna mpango wa ujenzi wa reli ya kisasa – SGR Tanga - Moshi - Arusha hadi Musoma, ndicho kitakachofuatia lakini treni hii haitasimama tena” Kadogosa alisema.
Hata hivyo abiria waliokuwa wakisafiri kutoka Dar es Salam kuelekea Arusha hawakuwa nyuma kuelezea furaha yao na hisia zao abiria hao walionekana na sura za furaha huku wakitoa shukrani zao za dhati kwa Serikali kupitia Shirika la Reli nchini kwa kurejesha usafiri wa treni ambao kwa takribani miaka 30 iliyopita ilikuwa imesimama kwa mkoa wa Arusha.
Hata hivyo, abiria wameeleza namna usafiri huu utakavyowasaidia katika shughuli nyingi za kibiashara na kilimo ambapo kwao itakuwa ni rahisi kusafirisha bidhaa na mazao kuleta Dar es Salaam ambapo ndio kitovu cha biashara nchini.