Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM AONGOZA VIONGOZI WA DINI KUTEMBELEA STESHENI YA SGR


news title here
05
October
2020

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Abubakar Kunenge akiambatana na viongozi wa Dini wa mkoa wa Dar es Salaam wametembelea jengo la Stesheni ya reli ya kisasa – SGR lililopo Jijini Dar es Salaam Oktoba 5, 2020.

Mkuu wa mkoa ameandaa ziara hiyo yenye lengo la kuwapa fursa viongozi wa dini kutembelea miradi mbalimbali nchini ukiwemo mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa ambapo wamejionea Jengo hilo la stesheni lililojengwa kwa mfano wa madini ya Tanzanite sambamba na daraja refu la treni lililoanzia Stesheni hapo hadi eneo la Ilala jijini Dar es Salaam.

Ujenzi wa jengo hilo umefikia zaidi ya 90% huku mradi wenyewe kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro ukiwa zaidi ya 90%, kukamilika kwa jengo hilo mbali na shughuli za kiusafiri pia litatumika kama kituo cha biashara ambapo wananchi watapata fursa ya kuwekeza biashara za Migahawa, Hoteli, Mabenki na huduma nyingine za muhimu kwa ajili ya abiria na wananchi watakaokuwa wanafika katika kituo hiko.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ameipongeza Serikali ya awamu ya tano na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa ukuaji wa uchumi na maendeleo ya nchi kupitia ujenzi wa miundombinu ya kutosha ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa ambao unasimamiwa na Shirika la Reli Tanzania – TRC .
“Rais wetu anawapa kipaumbele sana viongozi wa Dini, na haya tunayojionea ni matunda ya maombi yao” alisema Mhe. Kunenge.

Naye Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Alhaji Mussa Salum amewaasa wananchi waendelee kuunga mkono juhudi za serikali katika kuleta maendeleo ya nchi kwa kuilinda miradi mikubwa inayoondelea kujengwa ukiwemo mradi huo wa SGR ambao utaleta manufaa makubwa kwa taifa na wananchi.

Mkurugenzi wa Miundombinu ya Reli TRC Mhandisi Faustine Kataraia amesema kuwa Jengo hilo liko mbioni kukamilika kwa kumalizia vifaa vya ndani vya usalama, mawasiliano na umeme ambavyo vitaendesha kazi za stesheni hiyo.

Aidha, Mhandisi Kataraia alifafanua faida zilizopatikana kutokana na ujenzi wa mradi huo kwa kuwapatia ajira za moja kwa moja watu elfu 14 pamoja na elfu 80 ambazo si za moja kwa moja kama vibarua wa kupakia michanga, nondo, mathalan mifuko ya nafaka Milioni 9 itatumika katika mradi huo ambayo ni sawa na Tani laki moja na kumi na tano elfu na pia wakandarasi wadogo 971 ambao wanasafirisha Saruji, kuleta vyakula, Nondo na bidhaa nyingine katika mradi huo.

Pia Mhandisi Kataraia ameelezea ujenzi wa kiwanda cha utengenezaji wa mataruma kilichopo Kilosa Mkoani Morogoro ambacho kinazalisha Mataruma zaidi ya elfu moja kwa siku
“Katika mradi huu tutatumia jumla ya Mataruma 1,200,000 na yote tutazalisha wenyewe na pia tutatumia mifuko ya saruji milioni mbili laki nne” aliongeza Mhandisi Kataraia.

Vilevile alisema kuwa mradi huo utatumia nishati ya umeme na upo wa kutosha, umeme utachukuliwa moja kwa moja kutoka katika mhimili wa taifa kutoka Kinyerezi pamoja na na vyano vingine vya Shirika la Usambazaji Umeme - TANSECO, hivyo wananchi wasiwe na hofu juu ya uendeshaji wa mradi huo pindi utakapoanza.