Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

MKURUGENZI MKUU TRC ATAKA WATUMISHI KUWAJIBIKA NA KUFANYA KAZI KWA BIDII


news title here
11
February
2025

Mkurugenzi Mkuu Shirika la Reli Tanzania Ndugu Masanja Kungu Kadogosa, Februari 10, 2025 amefunga mafunzo ya weledi kwa waajiriwa wapya wa Shirika la Reli Tanzania - TRC yaliyofanyika ukumbi wa Gerezani Jijini Dar es Salaam.

Mafunzo hayo ya siku saba yenye lengo la kuwafundisha watumishi misingi, malengo, maadili, miko na taratibu za kazi katika utumishi wa Umma yameshirikisha waajiriwa wapya 221 wa kada mbalimbali zikiwemo kada za stesheni masta (30), fundi sanifu (40), mafundi mchundo (109), afisa biashara (1), madereva mitambo (33), uhandisi(2) na Yadi masta (6).

Akiongea wakati wa hafla ya ufungaji mafunzo elekezi Mkurugenzi Mkuu TRC Ndugu Masanja Kungu Kadogosa amewataka wafanyakazi wa Shirika la Reli Tanzania kuthaminiana ili kuleta tija na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi na utekelezaji wa majukumu.

"Kila mmoja ana thamani na ujuzi wake, kazi ya kila mtu inategemewa ili kufanikisha kazi ya mwingine katika Shirika, hivyo ni lazima uthamini kazi yako, haijalishi umeanza na kazi gani cha msingi unaona nini mbele yako, unaweza ukawa Mkurugenzi wa TRC siku moja" alisema Ndugu Kadogosa.

Aidha, Kadogosa amewataka wafanyakazi wapya kufuata kanuni na misingi ya kiutumishi ili kuepusha migogoro na uvunjifu wa Sheria na Kanuni za utumishi.

"Sisi tunaitwa watumishi wa umma, tofauti yetu na Taasisi au mashirika binafsi ni katika maadili, tunapokuwa huku tunafanya kazi ya Serikali na kuhudumia wananchi wote, hivyo ni lazima kuzingatia maadili, utaratibu, kanuni, Sheria na misingi ya kiutumishi" amesema Kadogosa.

Naye Mkurugenzi wa Rasilimali watu na Utawala Shirika la Reli Tanzania Bi. Irene Ungani-kyara ameeleza kuwa mafunzo yaliyotolewa yamejikita katika kuhakikisha watumishi wanazifahamu kanuni za kiutumisha za utendaji kazi, idara mbalimbali zinazoliunda Shirika pamoja na majukumu ya idara hizo na masuala yanayohusu afya ya akili na athari zake ili kuwafanya wafanyakazi watekeleze majukumu kwa weledi na ufanisi.

"Taasisi yetu inatoa huduma kwa wananchi, na sisi kama watumishi wa umma kama hatutakuwa na uelewa wa masuala ya kiutendaji itachangia kuzorotesha huduma na ufanisi hafifu" alisema Bi. Irene.

Bestina Jomanga mwajiriwa mpya wa Shirika la Reli Tanzania amesema kuwa mafunzo ya uelewa yatamsaidia katika kuhakikisha anawajibika na kuwahudumia wananchi kwa weledi na ubunifu wa hali ya juu.

"Nimejifunza namna ya uwajibikaji na kuhudumia Jamii, Taasisi na Shirika, nimepata elimu jinsi gani tunapaswa kutoa huduma bila upendeleo na hilo nimezingatia" amesema Bestina.

Shirika la Reli Tanzania Linaendelea kuwahudumia wananchi wote kwa weledi na kwa kufuata kanuni na misingi ya utoaji huduma ili kuleta mafanikio ya kiuchumi kwa kila mtu na nchi kwa ujumla.