MKURUGENZI MKUU TRC ASHIRIKI MAHAFALI YA 27 YA SHULE YA MSINGI ITIGI RELI
September
2020
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika a Reli Tanzania Ndugu Masanja Kungu Kadogosa ashiriki katika sherehe ya mahafali ya 27 ya Shule ya Msingi ya Itigi Reli mkoani Singida hivi karibuni Septemba 2020.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na wadau mbalimbali wa shule ya Itigi Reli wakiwemo wazazi, wafanyakazi wa TRC, wanafunzi waliowahi kusoma katika shule hiyo pamoja na wawakilishi kutoka Wilaya ya Itigi ambapo mgeni rasmi alikuwa Afisa Elimu Sekondari Bwana Kelvin Ngonyani akimuwakilisha mkuu wa Wiaya ya Manyoni.
Shule ya Msingi Itigi Reli ilianzishwa mwaka 1987 lengo likiwa ni kutoa elimu kwa watoto wa wafanyakazi wa Shirika la Reli wanaofanya kazi katika maeneo ambayo hakuna shule za msingi au shule ziko mbali na maeneo wanayofanyia kazi, shule hii ilizinduliwa rasmi na Rais wa awamu ya pili Mhe. Ally Hassan Mwinyi Aprili 04, 1993 ikiwa chini ya umiliki wa Shirika la Reli.
Shirika limeendelea kumiliki na kuihudumia shule hiyo tangu kuanzishwa kwake ambapo limekuwa likitoa huduma zote muhimu kwa wanafunzi ambapo katika kuendelea kuwasaidia watoto hao Shirika lilianzisha mpango wa kuwahudumia pia wanafunzi wanaofaulu kwenda Sekondari zilizo karibu wakitokea shuleni hapo katika upande wa Malazi na Makazi.
Katika Hafla hiyo Mkurugenzi Mkuu TRC akiambatana na Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala Bi. Amina Lumuli na maafisa wengine wa Shirika alipata nafasi ya kukagua Mabweni, Vyumba vya Madarasa pamoja mazingira ya shule hiyo kwa ujumla ili kuona namna ya kuendelea kuboresha mazingira ya shule hiyo ili iweze kuendelea kutoa elimu bora na kushika nafasi katika ngazi ya wilaya, mkoa, kanda na taifa.
Aidha, Mkurugenzi Mkuu ameahidi kuendelea kuboresha mazingira ya shule hiyo kwa kutatua changamoto zinazoikabili shule hiyo ili kuweka mazingira bora kwa ajili ya wanafunzi kujisomea, sambamba na ahadi hiyo Mkurugenzi Mkuu aikabidhi vitabu vya Hesabu na Kusoma kwa ajili ya wanafunzi wa Darasa lakwanza pamoja na kuchangia kiasi cha Shilingi laki 5 kwa ajili ya motisha kwa walimu na wanafunzi.
Wazazi wa wanafunzi na wanafunzi wanaohitimu elimu ya msingi katika shul hiyo ewameeleza furaha yao kwa kuwa sehemu ya shule hiyo na kujivunia mafanikio yanayopatiana katika shule hiyo kutokana ushirikiano mzuri uliopo kati ya Walimu, Wanafunzi, Wazazi na uongozi wa Shirika ulioiwezesha shule hiyo kushika nafasi ya kwanza kiwilaya na 18 kimkoa.
“Watoto wanaendelea vizuri, mazingira ya shule ni mazuri, kabla ya kuwepo shule hii tulikuwa tunahangaika sana kwa sababu wengine tunaishi sehemu ambazo shule ziko mbali, hivi sasa mambo yamekuwa mazuri watoto wanaendelea vizuri, wanasoma kama watoto wengine” alisema Bi. Situmai Rashid, mmoja kati ya wazazi wa wanafunzi wanaohiitimu
Kwa upande mwingine Nassor Said ambaye ni mmoja kati ya wanafunzi waliosoma shule hiyo mwaka 1991 -1997 na kupata fursa ya kuhudhuria mahafali hayo kwa niaba ya wengine amesema kuwa “lengo la kuja hapa ni kwa ajili ya kuwahamasisha watoto wetu ili waweze kufanya vizuri, lakini pia hatukuja hivi hivi, sisi pamoja na wenzetu tulijipanga tukachanga na tumefanikiwa kuleta jezi na mpira lakini pia tutaendelea kushiriki katika kuisaidia Shule hii na tunatarajia hivi karibuni kuleta Kompyuta na ‘printer’.”
Hivi sasa Shule ya Msingi Itigi Reli ina jumla ya wanafunzi 204 ambapo kati yao 92 ni wasichana na 112 ni wavulana, kwa kipindi cha miaka minne mfululizo shule hiyo imekuwa ikifanya vizuri katika ufaulu ambapo kuanzia mwaka 2016 hadi 2019 wastani wa ufaulu ulikuwa asilimia 100.