MHE. PROF. MBARAWA AWEKA JIWE LA MSINGI MRADI WA SGR MAKUTUPORA - TABORA
April
2022
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa aweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa – SGR kipande cha tatu Makutupora - Tabora Aprili 12, 2022.
Hafla hiyo imefanyika katika uwanja uliopo Cheyo “B” mkoani Tabora ikihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na taasisi binafsi
wakiwemo mawaziri mbalimbali, katibu mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Balozi wa Uturuki nchini, Mkuu wa mkoa wa Tabora, wakuu wa wilaya, Kamati ya Bunge ya Bajeti, kamati ya Bunge ya Miundombinu, Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi ya Bodi ya Wakurugenzi Shirika la Reli Tanzania – TRC, viongozi wa chama na serikali, viongozi wa dini pamoja na taasisi binafsi.
Taasisi nyingine zilizohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Mamlaka ya Usafiri wa Ardhini (LATRA), Benki ya TCB, Kampuni ya Mafuta GBP, Benki ya
CRDB, Kampuni ya Tigo, Benki ya NMB, BRAVO Logistics, Benki ya NBC, Kampuni ya Puma, Shirika la Posta, Kampuni ya AKO, Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Kampuni ya BAKHRESA, Kampuni ya KAMAL, SMH Rail na Shirika la Bima.
Akihutubia katika hafla hiyo Mhe. Mbarawa amesema kuwa ujenzi wa Reli ya Kisasa Makutupora – Tabora unahusisha ujenzi wa reli yenye urefu wa jumla ya kilomita 368 ambapo kilomita 294 ni njia kuu na kilomita 74 ni njia za kupishania, ambapo hamani ya mkataba wa ujenzi ni Dola za Marekani bilioni 1.908 sawa na Shilingi trilioni 4.406, muda wa ujenzi ni miezi 46 ikijumlisha muda wa majaribio.
Mhe. Prof. Mbarawa ameipongeza Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na Wafanyakazi wa Wizara na TRC na kuongeza kuwa Serikali itaendelea kutimiza wajibu wake wa kutoa fedha za utekelezaji wa miradi hii.
"Wajibu wetu ni kuhakikisha kuwa mnatekeleza majukumu yenu kwa weledi
na umahiri mkubwa. Mfanye kazi kwa uzalendo, kwa pamoja kama timu moja, kujituma, kuongeza ubunifu na kuzingatia miongozo ya serikali" amesema Prof. Mbarawa
Mkuu wa mkoa wa Tabora Mhe. Batilda Buriani ameishukuru Serikali kwa kuamua kutekeleza mradi mkubwa wa kimkakati mkoani humo unaokwenda kuzalisha fursa za ajira na uchumi katika mkoa wa tabora.
“Mhe Mgeni rasmi sisi tunatambua kuwa kuna fursa nyingi katika mradi huu, nakuahidi kwamba tutaulinda mradi huu, tutashirikiana na TRC
katika kulinda miundombinu pia katika kuhakikisha maeneo yanapatikana ili mradi uendelee, na mimi sina wasiwasi na TRC kwasababu TRC wamedhihirisha kuwa wanajali eneo wanalofanyia kazi ndio maana TRC leo wametupa eneo kwaajili ya wajasiriamali” amesema Mhe. Batilda
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Masanja Kadogosa katika taarifa yake ameeleza kuwa kipande cha SGR Makutupora – Tabora kitakuwa na vituo vya abiria na mizigo vipatavyo nane (8) ambavyo ni Manyoni, Itigi, Kazikazi, Tura, Malongwe, Goweko, Igalula na Tabora, pamoja na kituo cha uendeshaji treni cha dharura Tabora, hii ni endapo ikitokea hitilafu katika kituo kikuu (OCC) Dar es salaam treni ziweze kuongozewa kutokea tabora bila kusimamisha kazi za uendeshaji.
Miongoni mwa faida mabazo wananchi wa mkoa wa Tabora watazipata kupitia mradi wa SGR ni pamoja na ajira ambapo Kwa takwimu zilizopo,
mpaka sasa jumla ya ajira za moja kwa moja zimetolewa kwa watanzania 16,000. Pia, Ajira hizo zimechangia malipo ya mishahara yenye thamani ya Shilingi Bilioni 224, zabuni na kandarasi zenye thamani ya shilingi trilioni 1.776 zimetolewa kwa wakandarasi wadogo 1663. Faida nyingine ni kuwa serikali imekusanya kodi yenye jumla ya Shilingi bilioni 441.