Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​MAMA MONGELA, WAKONGWE WA TABORA GIRLS WAPANDA MCHONGOKO KUUONA MJI WA SERIKALI MTUMBA


news title here
23
January
2025

Jumla ya wanawake 50 waliosoma shule ya sekondari ya Wasichana Tabora mwaka wakiongozwa na Getrude Mongela wametembelea mradi wa reli ya kisasa ya SGR, ambapo walianzia stesheni ya Magufuli jijini Dar es Salaam kisha kusafiri kwa treni ya umeme hadi Dodoma tarehe 23, Januari 2025.

Lengo la ziara ya kundi hilo maarufu kama "Warsaw" ni kuona maendeleo ya mradi wa SGR katika kipande cha kwanza Dar es salaam - Morogoro na kutoka Morogoro - Dodoma na kutembelea mji wa kisasa wa kiserikali Mtumba jijini Dodoma.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo Mama Mongela, amesema usafiri wa Treni za abiria za SGR ni usafiri salama na wenye uhakika kwani unazingatia muda kufuatia treni kutoka kwa wakati na kufika kwa wakati hivyo kumfanya abiria kufika kwa wakati na kutekeleza majukumu yake inavyotakiwa.

"Naipongeza Serikali ya Tanzania pamoja na wafanyakazi wote wa TRC kuwezesha usafiri huu muhimu aidha napenda niwasisitize abiria kuendelea kutumia treni hii ikiwamo kulinda vitendea kazi vyote ili kudumisha usafiri huu, pia nasisitiza wafanyakazi wa TRC waendelee kuelimisha wananchi kulinda miundombinu ya reli" ameongeza Mama Mongela.

Naye Bi. Mwajuma Mchata amesema reli ya SGR itakapokamilika, itarahisisha kuweka mawasiliano na nchi jirani ikiwemo Congo, Rwanda na Burundi ambapo Tanzania itakua inasafirisha mizigo ya wafanyabiashara kutoka Bandari ya Dar es salaam kwenda katika nchi hizo na hii itakuza uchumi wa nchi yetu na itakuza maendeleo nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa TRC Masanja Kungu Kadogosa, amesema kwa sasa Shirika linategemea kusaini mkataba wa ujenzi wa reli ya SGR kutoka Uvinza - Musongati kwaajili ya kuunganisha Tanzania na Burundi na hii itachangia ukuaji wa uchumi nchini kupitia usafirishaji wa mizigo.

"Kimkakati TRC imejipanga kuifikia miji mikubwa mitatu ya Jamhuri ya Demokrasia ya Congo kwaajili ya kufanya nao biashara na ikumbukwe reli ndo usafiri nafuu zaidi" amesisitiza Kadogosa.

Shirika la Reli Tanzania linaendelea kusimamia ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Makutupora - Tabora, Tabora - Isaka, Isaka - Mwanza na Tabora hadi Kigoma.