MAJARIBIO YA MIFUMO YA UMEME KATIKA RELI YA KISASA (SGR ) DAR- MORO YAANZA RASMI

April
2022
Shirika la Reli Tanzania – TRC kwa kushirikiana na Mkandarasi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa – SGR kampuni ya Yapi Merkezi limeanza zoezi la majaribio ya mifumo ya umeme katika miundombinu ya reli ya kisasa Pugu jijini Dar es Salaam Aprili 27, 2022.
Zoezi hilo ni sehemu ya majaribio ya mifumo ya umeme kwa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro ambacho kipo katika hatua za mwisho za ujenzi kwaajili ya kuanza shughuli za uendeshaji. Uwashaji umeme katika reli ya kisasa unafanyika kwa awamu nne katika vituo vinne vya kupozea umeme ambapo uwashwaji umefanyika kwa mafanikio katika kituo cha kwanza kilichopo Pugu.
Vituo vingine ni pamoja na kituo cha Ruvu, Ngerengere na Morogoro ambavyo vitawashwa kwa awamu huku zoezi la kupitisha kichwa cha treni cha Mkandarasi kinachotumia umeme likifanyika kwa utaratibu huo. Lengo la majaribio yanayofanywa na mkandarasi ni kuhakikisha kuwa mifumo yote iliyopo kwenye reli ya kisasa iko sawa na tayari kwaajili ya shughuli za uendeshaji bila ya kuleta madhara kwa watumiaji.
Aidha, Shirika kwa kushirikiana na Mkandarasi linaendelea na zoezi la utoaji elimu na kuhamasisha jamii kuhusu tahadhari za kuchukua na taratibu za kufuata wakati wa majaribio ya mifumo ya umeme katika reli ya kisasa.
Maeneo ambayo tayari elimu hiyo imetolewa kwa wananchi ni pamoja na Mtaa wa Guluka kwa lala, Gongo la mboto, Buguruni Sokoni, Vingunguti, Kwa Mnyamani, Kipawa mji mpya, Majumba sita, Shule ya Sekondari Ilala, Majani ya chai, Pugu stesheni, Pugu Mnadani, Sekondari ya Ukonga, Shule ya msingi Mikongeni, kata ya Gongo la Mboto, Mwembe Madafu, Ruvu na Soga.
Katika zoezi hilo wananchi wameendelea kulishukuru Shirika la Reli Tanzania kwa kujali afya na usalama wa wananchi kwa kuwapa elimu ya ulinzi na usalama katika kipindi cha majaribio ya miundombinu ya umeme wa reli ya kisasa.
Yusta Peter, mwanafunzi wa shule ya sekondari Ilala amesema kuwa "Napenda kulishukuru Shirika la Reli Tanzania kwa elimu kuhusu mradi wa SGR bila kutuelimisha tusingejua madhara ya kutozingatia usalama, cha muhimu ni wanafunzi kuzingatia mafunzo na kufuata miongozo wanayopewa ili waweze kutimiza ndoto zao"
Naye mkazi wa Gongo la Mboto Bwana Nikaro Sabai amesema kuwa “Elimu inayotolewa ni muhimu sana na ningeliomba Shirika liendelee na elimu hii ya usalama na mara kwa mara kwasababu ujenzi wa reli ya kisasa ni kitu kipya kwa jamii kwahiyo tunahitaji elimu madhubuti ili tuweze kujenga utamaduni wa kutunza na kuzingatia usalama wa reli"
Katika kuhakikisha usalama unazingatiwa ni vyema kila mwananchi kuchukua hatua madhubuti katika kufuata sheria na miongozo inayotolewa ikiwemo namna ya kuvuka kwenye miundombinu ya reli, kutoa taarifa sehemu sahihi pindi changamoto za kiusalama zinapotokea na kujenga utamaduni wa kutunza miundombinu ya reli kwa manufaa ya Taifa.