Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

MAJARIBIO AWAMU YA PILI TRENI ZA SGR YAFANA, MABEHEWA 14 YAFUNGWA


news title here
18
March
2024

Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa ameshuhudia majaribio ya treni ya reli ya kiwango cha kimataifa - SGR yenye mabehewa 14 kwa kusafiri ndani ya treni kutoka stesheni ya Dar es Salaam hadi Morogoro, Machi 18, 2024.

Lengo la Waziri wa Uchukuzi kusafiri na treni ya SGR ni kufanya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa SGR sambamba na kujionea maandalizi na utayari wa watumishi na vitendea kazi vitakavotumika kwenye uendeshaji wa huduma za SGR hivi karibuni.

Mhe. Mbarawa amesema kuwa kwa sasa majaribio ya treni za SGR yanaendelea katika hatua mbalimbali za kitaalamu ili kuhakikisha usalama kabla ya kuanza kusafirisha abiria na mizigo.

"Haya majaribio sio ya kwanza, majaribio yalianza mwezi Novemba 2023 kwa majaribio ya kichwa cha treni na sasa tunafanya majaribio ya kichwa cha treni kuvuta mabehewa, majaribio ya kwanza yalianza na mabehewa manne na leo hii tumefunga mabehewa 14" amesema Prof. Mbarawa

Aidha, Mhe. Mbarawa amepongeza jitihada zinazofanywa na wataalamu wa Shirika la Reli Tanzania - TRC ambao wameweza kufanikisha majaribio ya awamu ya pili kwa kiasi kikubwa kuliko ilivotarajiwa.

"Nichukue fursa hii kuipongeza timu ya TRC, majaribio ya awali ya treni ilikuwa ikitembea kwa wastani wa mwendokasi wa kilomita 110 mpaka 120 kwa saa, kadiri majaribio yanavofanyika uboreshaji unaendelea na leo tumetembea kilomita 150 kwa saa ndani ya saa mbili kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro" amesema Mhe. Mbarawa.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima amesema anaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali za ujenzi wa SGR ambao utaenda kukuza uchumi wa mkoa wa Morogoro kupitia sekta ya kilimo na utalii.

"Sisi watu wa Morogoro suala la SGR linakuja na neema nyingi sana ,kwa upande wa pili wa stesheni ya Morogoro tumejenga kituo cha mizigo (cargo terminal), lengo letu ni kupunguza msongamano barabarani, vilevile stesheni ya Kilosa itatumika na watalii wanaokwenda mbuga za Mikumi na Udzungwa, hii yote inaonesha ni jinsi gani tunaamini SGR ni uti wa mgongo kwa mkoa wa Morogoro" amesema Mhe. Malima.

Mkurugenzi Mkuu TRC Ndugu Masanja Kadogosa amesema kuwa TRC imeendelea kuhakikisha ujenzi wa miundombinu ya SGR unakamilika kwa wakati na majaribio ya kuhakiki usalama yanafanyika na ifikapo mwanzoni mwa mwezi Julai treni za SGR zitaweza kutembea kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma .

"Mhe. Waziri majaribio bado yanaendelea, ujenzi umekamilika kwa kipande cha kwanza kwa asilimia 98.98, sehemu kubwa iliyobaki ni njia ya kuingia bandarini lakini hiyo haituzuii kuanza shughuli za uendeshaji, hii itatuwia kutekeleza maagizo ya Mhe. Rais kwamba ifikapo Julai tutaweza kusafirisha abiria kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma" amesema Kadogosa.

Ujenzi wa mradi wa kimkakati wa SGR unaendelea katika vipande vyote kwa asilimia tofautitofauti ambapo kipande cha kwanza Dar Es Salaam - Morogoro kimekamilka kwa asilimia 98.90, kipande cha pili Morogoro - Makutupora asilimia 96.35, kipande cha tatu Makutupora - Tabora asilimia 13.98 , kipande cha nne Tabora - Isaka asilimia 5.44 , kipande cha tano Mwanza - Isaka asilimia 54.01 na kipande cha sita Tabora - Kigoma kikiwa katika hatua za maandalizi za kuanza kwa ujenzi.