Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

MAGINDU NA KWALA MKOANI PWANI WAPOKEA ELIMU YA ULINZI WA MIUNDOMBINU YA RELI SGR NA MGR


news title here
09
December
2024

Maafisa kutoka Shirika la Reli Tanzania - TRC kwa kushirikiana na viongozi wa vijiji wa mkoa wa Pwani wakiwemo maafisa watendaji, wenyeviti, Diwani wa Kata ya Kwala na afisa tarafa wa tarafa ya Ruvu, kwa pamoja wamefanya zoezi la ushirikishaji linalolenga uhamasishaji ulinzi wa miundombinu ya reli katika Kijiji cha Magindu, Kwala mkoani Pwani tarehe 08 mwezi Disemba 2024.

Wananchi wameelezwa kuwa jukumu la ulinzi wa miundombinu ya reli ikiwemo mataluma, reli pamoja na vitendea kazi yakiwemo mabehewa na vichwa vya treni ni la kila mwananchi hivyo waache kupiga mawe treni, kukata nyaya za umeme kwenye reli ya SGR, waache kuchoma moto kandokando ya reli na kulisha mifugo kandokando ya reli kwani watasababisha hasara kubwa kwa TRC pamoja na abiria wanaotumia usafiri wa reli ikiwemo uharibifu wa miundombinu, uharibifu wa mabehewa na vichwa vya treni kwani wanaweza kusababisha ajali itakayogharimu maisha ya wateja au abiria wanaotumia usafiri wa reli.

Diwani wa kata ya Kwala Mhe. Mansoor Ali Kisebengo ameiomba TRC kwa kushirikiana na TARURA kupokea changamoto zinazowasilishwa na wananchi ili kuzitatua ili kusaidia kuweka usawa katika jamii hususani maombi ya barabara katika eneo la Kwala - Ruvu - na Kwala - Msua kwani barabara hii itawezesha wananchi wa Kwala kwenda kukata tiketi na kupanda treni za SGR Ruvu Stesheni pamoja na kufanya shughuli zingine za kiuchumi na kijamii kati ya Kwala, Ruvu na Msua.

"Tunaomba mawasiliano kati ya Kwala, Ruvu na Msua yarudi kwaajili ya kuboresha na kuendeleza huduma za kijamii na kiafya hususani kwa wananchi wa Msua kwani hutibiwa Zahanati ya Afya Kwala, hutumia kituo cha polisi Kwala katika masuala ya kiusalama na wanafunzi husoma Kwala" ameongeza Mhe. Kisebengo.

Mhe. Diwani Kisebengo pia ameipongeza TRC kwa kuweza kuwafikia wananchi wa Kwala na kuwapa elimu shirikishi ya umuhimu wa utunzaji wa miundombinu ya reli pamoja na kua walinzi wa mali za umma nchini.

Mkazi wa Kijiji cha Magindu Ernest Yohana ameipongeza TRC kwa kuwezesha zoezi shirikishi na amesema atakuwa balozi mzuri kwa kushirikiana na vijana wenzie katika kuhakikisha miundombinu inakua salama na inalindwa, vilevile ameiomba serikali na TRC kuwarekebishia barabara wananchi walioguswa na mradi wa reli ya kisasa kwaajili ya kuwasaidia kufika stesheni ya Ngerengere na kufanya shughuli zingine za maendeleo kupitia barabara hizo.

Huu ni muendelezo wa TRC wa kufanya kampeni za uelewa kwa wananchi wa maeneo husika mara kwa mara kwa kushirikiana na viongozi wa Serikali ikiwemo ofisi za wakuu wa Mikoa, wakuu wa Wilaya,viongozi wa kata, mitaa,vijiji ikiwemo vyombo vya habari vya asili, mitandao ya kijamii na vipeperushi kwaajili ya kumuwezesha mwananchi kuelewa umuhimu wa reli na usafiri wa treni katika kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.