Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​MAENEO ZAIDI YA ISHIRINI NA NANE YANUFAIKA NA MAFUNZO YA UJASIRIAMALI


news title here
02
March
2021

Shirika la Reli Tanzania – TRC limewanufaisha wananchi wa maeneo zaidi ya ishirini na nane kwa kutoa elimu ya mafunzo ya ujasiriamali na kujikwamua kiuchumi kwa wananchi waliotwaliwa na ardhi na kupisha mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa – SGR kipande cha kwanza Dar es Salaam – Morogoro, Februari 2021, hivi karibuni.

Kupitia mafunzo hayo TRC imeweza kuwaunganisha wananchi pamoja na wakufunzi mbalimbali kutoka katika eneo husika la mafunzo ili kuweza kuwarahisishia wananchi kutotumia gharama na muda mwingi wa kwenda sehemu yenye umbali tofauti na makazi yao kwaajili ya kupata mafunzo.

Wakufunzi hao ni pamoja na mafundi nguo, wachomea chuma, watengenezaji wa batiki , watengenezaji wa sabuni na mafuta, wakulima na wafugaji, watengenezaji wa nafaka pamoja na wajasiriamali wadogo waliotoka katika eneo husika la mafunzo ambapo walipata nafasi ya kutoa elimu juu ya fani zao kwa wananchi.

Afisa maswala ya kijamii kutoka TRC Bi. Tumaini Rikanga alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kumsadia mwananchi aliyetwaliwa na mradi kujikwamua na kujiendeleza kiuchumi kwakua wamejitoa kupisha mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa – SGR ili kukuza maendeleo ya nchi.

”Wananchi wamejitoa , hakika ni wazalendo hivyo hatuna budi sisi kama shirika kujitoa kwa ajili yao” alisema Bi. Tumaini.

Aidha Bi. Tumaini alitoa shukrani kwa wananchi kwa kuitikia wito na kupokea mafunzo hayo ikiwa ni njia mbadala ya kuongeza upeo na uwezo wa kufanya vitu tofauti kwaajili ya kujiingizia kipato na ujuzi kwakua elimu haina mwisho.

Naye fundi chuma Bw. Alila Bakari kutoka wilaya ya Kisarawe alisema kuwa hiyo ni fursa kubwa kwa wananchi kujifunza bila gharama yeyote na kupitia mafunzo hayo kunaweza kuibua maendeleo makubwa ya kibiashara katika maeneo mengi.

“Ninaamini serikali yetu ina nia nzuri na wananchi wake, ndio maana tunapata elimu nzuri zenye manufaa kwa jamii” alisema Bw. Alila.

Aidha mafunzo hayo ya ujasiriamali ni mafunzo yenye muendelezo yatakayotolewa kwa wananchi wa maeneo mbalimbali ambao wametwaliwa ardhi zao ili kupisha mradi wa reli ya kisasa - SGR kuanzia kipande cha kwanza Dar es Salaam- Morogoro hadi kipande cha pili Morogoro – Makutupora.