Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​KONGAMANO LA BIASHARA NA UWEKEZAJI KATIKA SEKTA YA RELI LAFUNGULIWA


news title here
05
March
2024

Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. David Mwakiposa Kihenzile amefungua kongamano la Biashara na Uwekezaji katika sekta ya reli linalofanyika kwa muda wa siku mbili katika ukumbi uliopo Hoteli wa Malaika jijini Mwanza kuanzia Machi 5 hadi 6, 2024.

Lengo la kongamano ni kuwakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji na kuwapatia maarifa kuhusu fursa za biashara na uwekezaji zilizopo katika sekta ya reli kupitia ‘Open Access’, na ‘Public Private Partnership’ ili kuongeza ufanisi katika utoaji huduma za usafiri wa abiria na usafirishaji mizigo kupitia reli.

Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. David Kihenzile ambaye ni Mgeni rasmi katika Kongamano alisema kuwa uwekezaji wa Serikali unaoendelea katika sekta ya reli ni jambo kubwa na baada ya miaka michache tutaona mabadiliko makubwa yaliyofanyika kupitia reli ya kiwango cha kimataifa - SGR yenye urefu wa kilomita 2200.

Pamoja na lengo kuu, kongamano limedhamiria kuibua fursa za biashara na uwekezaji zilizopo katika maeneo ambayo reli ya zamani (MGR) na reli ya kiwango cha kimataifa (SGR) zimepita ili kuchochea maendelea ya sekta nyingine ikiwemo madini, kilimo, utalii, ufugaji na uvuvi, hatimaye kuleta maendeleo ya mwananchi na taifa kwa ujumla.

“Kwa jitihada zinazoendelea ni wazi kwamba Serikali inataka kuwa na uchumi ambao kila mwananchi atakuwa sehemu ya maendeleo ambapo mtu anaweza kujenga kiwanda kokote nchini ambako reli inapita na akayafikia masoko ya Dar es Salaam kupitia reli ya kiwango cha kimataifa” alisema Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania, Masanja Kadogosa.

Kongamano limehudhuriwa na wakuu wa mikoa ambayo reli imepita, taasisi za umma, sekta binafsi, wasafirishaji na wawekezaji, pamoja na wawezeshaji kutoka ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kutoa mada mbalimbali ambapo kwa muda wa siku mbili washiriki watapata fursa ya kufahamu kuhusu biashara na uwekezaji katika reli kupitia mada na majadiliano.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Prof. Godius Kahyarara alisema kuwa baada ya kongamano hili la biashara na uwekezaji wa reli, miezi mitatu kutoka sasa tutakuwa na biashara na uwekezaji makini katika mtandao wa reli nina uhakika kabisa kuna vitu vizuri na vikubwa vya uwekezaji vitapatikana, ninawashukuru TRC kwa kuona umuhimu wa kuimarisha reli ili kuunganisha bandari zetu.

“Tunashukuru wakuu wa mikoa wamefanya kazi kupitia wasaidizi wao hasa makatibu tawala na wakurugenzi sehemu zote ambako SGR impeita, wamekuwa wakitupatia taarifa hizi na tumekuwa tukiwapelekea wawekezaji, wengine wapo hapa kwenye kongamano, bahati nzuri sana mkoa wa Pwani na Morogoro una watu wengi walioonesha nia ya kuingia kwahiyo tukasema hii ni fursa sasa wenye mikoa wataona” aliongeza Prof. Kahyarara.

ongamano la Biashara na Uwekezaji katika sekta ya reli ni sehemu ya maandalizi ya kuanza uendeshaji wa huduma za treni katika reli ya kiwango cha kimataifa ambazo zinatarajiwa kuanza mwezi Julai 2024 kufuatia maelekezo ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanza huduma ifikapo Julai 2024. Pamoja na kongamano, Shirika linaendelea na maandalizi ikiwemo kupokea vitendea kazi, mafunzo ya wataalamu na majaribio ya vichwa na mabehewa ya treni.