Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​KAMPENI YA UELEWA KWA JAMII KUHUSU UJENZI WA SGR YAZIDI KUSHIKA KASI MAKUTUPORA – TABORA


news title here
25
April
2022

Shirika la Reli Tanzania TRC, limeanza kampeni maalumu ya uelewa kwa jamii kuhusu mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa - SGR, kipande cha tatu cha Makutupora – Tabora, ikihusisha mikoa ya Singida na Tabora ambayo inapitiwa na mradi, Aprili 2022.

Kampeni hiyo iliyoanza mapema mwezi Aprili, mkoani Singida, inahusisha timu ya wataalamu kutoka idara mbalimbali za TRC kwa lengo la kutoa uelewa kwa Viongozi na wananchi katika mikoa hiyo kuhusiana na masuala ya fursa za ajira na biashara, elimu ya awali ya utwaaji ardhi na fidia, ulinzi na usalama, mazingira na masuala mtambuka yatakayoambatana na mradi.

Akizungumza mara baada ya mkutano wa hadhara na wananchi wa mji mdogo wa Manyoni, wilayani Manyoni mkoani Singida, afisa kutoka Kitengo cha Usimamizi wa masuala ya kijamii, Bw. Leodgard Otaru amesema kuwa kwa mkoa wa Singida Kampeni hiyo imefanyika kikamilifu katika Halmashauri ya mji Itigi na halmashauri ya mji Mdogo wa Manyoni na inatarajiwa kufanyika mkoani Tabora kuanzia tarehe 25 Aprili 2022.

“wananchi wamepokea vizuri kampeni hii na wameonesha ushirikiano mkubwa, kwani katika baadhi ya maeneo wameruhusu mkandarasi aendelee na shughuli za awali za utekelezaji wa mradi kama vile uchukuaji wa sampuli za udongo” aliongeza Bw. Otaru.

Kampeni ya uelewa kuhusu mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa, imekuwa ni moja kati ya hatua muhimu za utekelezaji wa wa mradi huu wa kimkakati ambapo kwa kupitia mikutano ya hadhara wananchi na viongozi wanapata taarifa sahihi za mradi na hatimaye kurahisisha utekelezaji.

Pamoja na wataalamu kutoka TRC, kampeni ya uelewa kuhusu Mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa inajumuisha pia wawakilishi kutoka kampuni ya mkandarasi, akizungumza katika moja ya mikutano ya hadhara wilayani Manyoni, Afisa Uhusiano kutoka Kampuni ya Mkandarasi Yapi Merkezi, Bi. Hamisa Juma ameeleza kuwa pamoja na kutekeleza shughuli za ujenzi katika mradi, mkandarasi pia ana jukumu la kusaidia katika baadhi ya changamoto zinazoikumba jamii inayoishi kando na mradi.

Bi. Hamisa amesema kuwa “utaratibu ni kwamba baada ya kutambua changamoto wanayohitaji mkandarasi asaidie kuitatua, wananchi wawasilishe taarifa katika uongozi wa kijiji ambao utaandika barua kwenda kwa mkandarasi”.

Mmoja wa wakazi wa mji Mdogo wa Manyoni, Bi. Sarah Mwampeta ameeleza kuwa wamepokea vizuri ushirikishwaji wa wananchi kupitia kampeni ya uelewa.

“mradi huu utawapatia ajira vijana katika haya maeneo yetu, lakini pia reli ya kisasa itaturahisishia usafiri ukilinganisha na reli ya zamani ambayo tulikuwa tunasafiri kwa muda mrefu”

Sambamba na zoezi la Kampeni ya uelewa kwa jamii, hatua za awali za ujenzi wa reli ya kisasa Makutupora – Tabora zinaendelea ikiwa ni pamoja na Utambuzi wa maeneo ya ujenzi wa Makambi, ukusanyaji wa mitambo na rasilimali watu pamoja na uchukuaji wa sampuli za udongo katika maeneo ya Kitaraka, Itigi mjini na Kazikazi.

Kampeni hii inafuatia kuanza rasmi kwa shughuli za ujenzi katika kipande cha SGR Makutupora – Tabora ambapo tarehe 12 Aprili 2022, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, aliweka jiwe la msingi katika eneo la Cheyo B mkoani Tabora.