Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​KAMATI YA MIUNDOMBINU YATOA HEKO KWA TRC USIMAMIZI BORA MRADI WA SGR


news title here
15
March
2024

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu yalipongeza Shirika la Reli Tanzania - TRC kwa usimamizi bora wa mradi wa ujenzi wa Reli yenye kiwango cha kimataifa - SGR kufuatia ziara ya ukaguzi wa mradi wa SGR kutoka Tabora hadi Mwanza, Machi 2024.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Ndugu Selemani Kakoso alisema kuwa jitihada zinazofanywa na serikali kupitia TRC zimefanya mradi huo kuwa wa kiwango na utanufaisha watanzania.

“Serikali tunaipongeza kwa kutoa fedha nyingi, kwani katika miradi ambayo Serikali inatoa fedha za uhakika ni mradi wa SGR” alieleza Ndugu Kakoso.

Aidha, Ndugu Kakoso alisema kuwa Kamati imefanya ziara ya kipande cha kwanza cha Dar es Salaam - Morogoro na kujiridhisha hivyo kuendelea kukagua vipande vingine vya mradi.

“Tuwaombe watanzania waamini kuwa Reli ambayo imeahidiwa na serikali ya awamu ya sita inaonesha dalili kwamba itakamilika na kupeleka kwenye matawi yale yaliyokusudiwa” alisema Ndugu Kakoso.

Naye Mkurugenzi Mkuu kutoka TRC Ndugu Masanja Kadogosa alieleza kuwa kwa kipande cha tano Isaka - Mwanza mradi umefikia asilimia 54 ambapo sehemu kubwa ikiwemo tuta la reli limefikia zaidi ya asilimia 80, madaraja yamefikia zaidi ya asilimia 80.

“Kipande hiki cha tano ndicho Mhe. Rais alianza nacho na tunaimani kubwa kitamalizika mapema kuliko vipande vilivyobakia” alisema Ndugu Kadogosa.

Kamati ya Bunge ya Miundombinu ilipata fursa ya kutembea kwenye reli kwa kutumia kiberenge cha mkandarasi kutoka mkoani Shinyanga hadi Malampaka mkoani Simiyu.