KAMATI YA BUNGE YA MIUNDOMBINU YATOA HEKO KWA TRC KUSIMAMIA VYEMA MIUNDOMBINU YA RELI

March
2025
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imelipongeza Shirika la Reli Tanzania (TRC), kwa kusimamia vyema miundombinu ya reli ya SGR na MGR walipotembelea stesheni ya Tanga kwenye reli ya Kaskazini Machi 14, 2025.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Moshi Selemani Kakoso, alisema kuwa Serikali ina dhamira ya dhati ya kuunganisha mikoa mitatu ya kanda Kaskazini kupitia ukarabati wa reli ya kutoka Ruvu kuelekea Tanga, Kilimanjaro na Arusha.
"Kwakweli reli hii ni muhimu kwani itapunguza gharama za maisha na itafungua uchumi mkubwa kwa maeneo haya, Serikali haiwezi kujenga reli ya SGR maeneo yote” alisema Mhe. Suleiman Kakoso.
Aidha, Mhe. Kakoso alieleza kuwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan aliwaamini vijana wa TRC kusimamia na kujenga reli ya SGR kwa gharama ndogo na hawakumwangusha.
“TRC imejenga reli ya SGR kwa gharama nafuu ukilinganisha na wenzetu wa nchi jirani” aliongezea Mhe. Kakoso.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa TRC Bw. Focus Sahani, ameeleza kuwa TRC inaendelea na mpango mkakati wa kufufua reli ya Tanga kwenda bandari ya Tanga licha ta reli hiyo kuendelea kutoa huduma ya usafiri kutoka Dar es Salaam, Korogwe, Moshi na Arusha.
Aidha, Bw. Focus Sahani amesema kuwa TRC imeshapokea mabehewa ya mizigo 264 yatakoyotumika katika treni ya SGR ambayo yataongeza ufanisi wa ubebaji mizigo kwenda Dodoma.
“Reli ya SGR ikikamilika hadi kipande cha Mwanza itachukua muda wa saa tisa hadi kumi, hapo utaona jinsi usafiri utakavyokua rahisi” alisema Bw. Focus Sahani.
TRC inaendelea kusimamia vyema miundombinu ya reli ya SGR na MGR na kuendeleza mikakati ya ukarabati wa reli ya kaskazini na kuiongezea mwendokasi ambapo TRC imesaini mkataba wa ukarabati na kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation - CCECC kutoka nchini China.