Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

KAMATI YA BUNGE YA MIUNDOMBINU YAKAMILISHA ZIARA YAKE KUKAGUA MRADI WA SGR NA KARAKANA


news title here
14
March
2021

Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu yakamilisha ziara ya siku mbili kukagua Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa Dar es Salaam - Makutupora na Karakana ya reli mkoani Morogoro, ziara hiyo imefanyia kuanzia Machi 12 - 13, 2021.

Ziara hiyo ilikuwa na lengo la kufanya tathmini ya utekelezaji wa bajeti ya miundombinu pamoja na kuweka mikakati ya kutetea bajeti ya miundombinu katika bunge la bajeti linalotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Aidha, kamati imeridhishwa na utendaji wa Shirika hususani katika usimamizi wa miradi ukiwemo mradi wa SGR kutoka Dar es Salaam hadi Makutupora ambapo kwa kipande cha Dar es Salaam - Morogoro ujenzi wake umefika zaidi ya 90% ukitarajiwa kukamilika Agosti 2021 na kipande cha Morogoro - Makutupora ambacho ujenzi wake umefika 56%, halikadhalika mradi wa ukarabati wa vichwa sogeza 7 ambavyo vimekamilika tayari kwa ajili ya kuanza kazi.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Ndugu Masanja Kadogosa amesema kuwa lengo la ziara hiyo ni kwa ajili ya kuona maendeleo ya mradi sambamba na matumizi ya pesa ambazo zilipitishwa na bunge ili kutekeleza mradi huo.

“Wizara yetu inahusika kiutendaji na bajeti ya miundombinu, leo tumepata ugeni huu tunashukuru kwa sababu hiki ni kipindi cha bajeti hivyo wanapokuja wanapata fursa ya kuona matumizi ya pesa walizopitisha katika bunge la bajeti lililopita na kuendelea kutetea bajeti ili kuendelea kutekeleza mradi huu” alisema Kadogosa

Mkurugenzi ameongeza kuwa bado Shirika linaendelea kusisitiza ushiriki wa wazawa katika mradi ambapo kwa hivi sasa katika kazi nyingi zinazoendelea wanaofanya na kusimamia kazi hizo ni wazawa, mfano mzuri ni katika kiwanda cha Mataruma ambacho wajumbe wameweza kujionea kuwa wafanyakazi wote wanaosimamia kiwanda hiko ni watanzania.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Selemani Kakoso ametoa Shukurani zake kwa Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali kwa kazi kubwa kwa kuwa kazi katika kipande cha Dodoma – Morogoro kinakwenda vizuri na kuongeza kuwa wanakamati wana imani kuwa fedha wanazoidhinisha Bungeni zinafanya kazi kwa ajili ya manufaa ya taifa.

Mhandisi Mwanaisha Ulenge, Mbunge wa Viti Maalumu mkoa wa Tanga na Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu amepongeza Shirika la Reli kwa usimamizi mzuri wa mradi huo kwa kuzingatia viwango pamoja na utendaji wa kazi za ujenzi katika mradi huo