Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

FIDIA ZA MAENEO YA NYONGEZA ZAZIDI KUWANUFAISHA WANANCHI MOROGORO NA DODOMA


news title here
15
September
2021

Shirika la Reli Tanzania – TRC limeendelea na zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi ambao maeneo yao yametwaliwa ili kupisha shughuli za Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa - SGR ikiwa ni maeneo ya nyongeza kwa kipande cha Morogoro – Makutupora ambacho ujenzi wake umefika zaidi ya asilimia 73, hivi karibuni Septemba 2021.

Zoezi hilo linaendeshwa na Maafisa kutoka TRC kwa kushirikiana na viongozi na maafisa watendaji wa maeneo husika ya mkoa wa Morogoro ambayo ni Kikundi, Kimambila, Mkwatani, Mkadage, Mwasa pamoja na mkoa wa Dodoma katika maeneo ya Igandu, Chilwana, Zuzu, Kigwe, Miganga, Bahi Nakulu, Bahi Sokoni na Bahi Mapinduzi.

Mtendaji wa kijiji cha Igandu mkoani Dodoma Bwana Jonalis Kibendera ameeleza kuwa wananchi wamekuwa na wasiwasi kwamba huenda malipo yangechelewa lakini ameishukuru Serikali kwa kufanikisha zoezi hilo na kuwapatia wananchi fidia ambazo zinakwenda kubadilisha maisha yao.

“Walikuwa na wasiwasi kwamba malipo haya yangechelewa, lakini naishukuru serikali, kwahiyo fedha hizi zitawasaidia kuleta maendeleo pia naushukuru mradi ambao umepita katika kijiji changu kwa sababu Stesheni hii (Igandu) itawasaidia kusafirisha mazao yao na kwenda kununua bidhaa kwa urahisi na kurudi kwa urahisi” alisema Bwana Jonalis.

Wilson Yona ni mmoja wa wananchi ambao wamepokea fidia katika kijiji cha Igandu mkoani Dodoma ambapo emeeleza faida za mradi na kuishukuru serikali kwa kuwapatia fidia na vifuta machozi ili kupisha ujenzi wa miundombinu ya reli ya kisasa
“Naishukuru Serikali nimepata fidia, mradi huu umewanufaisha watu wengi, vijana wengi wapo kwenye mradi huu na wengi wamefanikiwa kujenga nyumba kupitia mradi huu, tunaushukuru mradi huu na tunaishukuru Serikali pia” alisema Bwana Yona

Mwantumu Sahabni, mkazi wa Zuzu mkoani Dodoma amesema kuwa “Eneo langu mara ya kwanza limechukulia na likalipwa na limechukuliwa mara ya pili na nimelipwa, mradi huu utasaidia kutupunguzia muda wa safari na kurahishisha shughuli za kibishaara”

Aidha, maeneo ya nyongeza hutwaliwa kwa ajili ya shughuli za ziada za mkandarasi ambazo hazihusishi ujenzi wa tuta la reli ambalo kwa kiasi kikubwa eneo lake liko tayari kwa ajili ya ujenzi na tayari ujenzi unaendelea.