BODI YA WAKURUGENZI TCRA WAFURAHISHWA NA MAENDELEO YA MRADI WA SGR
April
2019
Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania – TCRA yafanya ziara katika mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa – SGR kipande cha Dar es Salaam- Morogoro hivi karibuni Aprili 2019.
Lengo kuu ni kuona maendeleo ya ujenzi na kutambua ushiriki uliopo kati ya TCRA na TRC katika mfumo mpya wa mawasiliano katika uendeshaji wa reli mpya ya SGR.
Katika ziara hiyo ya wajumbe wa bodi ya TCRA ikiongonzwa na Mwenyekiti Dkt. Jones A. Kilimbe walipata fursa ya kuona hatua mbalimbali za maendeleo ya ujenzi wa reli ya kisasa ambao umefikia zaidi ya asilimia 48 kwa awamu ya kwanza Dar es Salaam – Morogoro ambao unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2019.
Dkt. Jones A. Kilimbe amesema lengo la ziara ni kujifunza na kuona namna Mamlaka ya Mawasiliano nchini inavyoweza kushiriki katika mfumo wa mawasiliano ya reli katika uendeshaji wa treni za umeme ili kuleta ufanisi katika mawasiliano na uchukuzi.
Hata hivyo Dkt Jones amelipongeza Shirika la Reli nchini kwa kusimamia vyema mradi mkubwa wa kitaifa ambao ni kielelezo cha Taifa katika mapinduzi ya kiuchumi.
Aliendelea kusisitiza Mwenyekiti wa bodi “Tunazidi kuamini kwamba huu ni mradi mkubwa sana ninatamani watanzania wengi wangepata nafasi kama hii ili kuweza kutambua kuwa tunamradi ambao miaka 100 ijayo tunazungumzia kwa lugha tofauti kuwa ni mapinduzi makubwa katika usafiri wa reli”.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania – TCRA Mhandisi James M. Kilaba amesema kuwa Mamlaka ya Mawasiliano ina jukumu la utoaji masafa ya mawasiliano, na wapo tayari kuendelea kushirikiana katika utoaji masafa ya mawasiliano ya reli ambapo mpaka sasa mamlaka ya Mawasiliano imeshatoa masafa kwa Shirika la Reli na pindi mradi utakapokamilika wataendelea kushirikiana katika kuhakikisha mifumo ya mawasiliano inafanya kazi ipasavyo.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano TRC Mhandisi Felix Mutashobya ameishukuru bodi ya wakurugenzi TCRA kwa kutembelea mradi na kuona namna watakavyoshiriki katika uendeshaji wa reli kwa njia ya mawasiliano, pia ameiomba Mamlaka ya Mawasiliano, Shirika la Reli na Wizara ya Uchukuzi na Mawasiliano kushiriki kikamilifu katika kutoa elimu kwa jamii kuhusu mfumo wa mawasiliano wa reli kwa lengo la jamii kuhusika katika ulinzi wa miundombinu ya mawasiliano punde mradi itakapokamilika.