Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​BENKI YA MAENDELEO AFRIKA KUTOA SHILINGI BILIONI 231.3 KUFADHILI UJENZI WA SGR KUUNGANISHA BURUNDI NA DRC


news title here
23
February
2024

Serikali imesaini mkataba wa mkopo wa ufadhili wa mradi wa ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa SGR awamu ya pili kipande cha kutoka Tabora hadi Kigoma na Uvinza hadi Malagarasi, katika ukumbi wa Wizara ya fedha jijini Dar Es Salaam Februari 23, 2024.

Pamoja na mkataba wa mkopo wa Ufadhili wa SGR serikali pia imesaini mkataba wa kuiwezesha Benki ya maendeleo ya Kilimo Tanzania, ambapo mikataba yote miwili ikiwa na thamani ya Shilingi Bilioni 398.7 za kitanzania huku kati ya hizo Shilingi Bilioni 231.3 ni kwaajili ya ujenzi wa Reli.

Akizungumza mara baada ya Kusaini mikataba hiyo, Waziri wa fedha Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema kuwa “mahitaji ya fedha kwaajili ya awamu ya pili ya ujenzi wa Reli ya Kiwango cha SGR ni makubwa hivyo Serikali imekubaliana na AFDB kuidhamini Serikali kupata takriban Shilingi Trilioni 8.1 za kitanzania kama mkopo kutoka masoko ya mitaji ili kutekeleza dhamira ya serikali ya kuimarisha miundombinu ya uchukuzi nchini”.

Dkt. Nchemba aliongeza kuwa ujenzi wa awamu ya pili ya mradi wa reli ya kiwango cha SGR ni muhimu katika kurahisisha usafirishaji nchini Pamoja na kuimarisha mahusiano ya kidiplomsia kati ya Tanzania na nchi Jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Burundi.

Meneja Mkazi wa Benki ya Maendeleo Afrika Dkt. Patricia Laverley kuziunganisha nchi za Afrika kiuchumi ni moja kati ya vipaumbele vya kimkakati vya Benki hiyo, na kuwa ni Fahari kwao kuwa sehemu ya mradi wa miundombinu itakayoziunganisha nchi za Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

“Pia vipande hivi vya awamu ya pili ya ujenzi wa Reli ya kiwango cha SGR vitatumia nishati ya umeme ambapo itasaidia kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa, jambo ambalo ni Fahari sana kwetu” aliongeza Dkt. Laverley.

Mkataba huu ni ufadhili wa kwanza wa AFDB katika miradi ya ujenzi wa Reli ambapo benki hiyo imekuwa mdau mkubwa wa maendeleo nchini kwa kufadhili miradi ya mbalimbali ya maji, ujenzi wa Barabara na Kilimo.

Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa ameishukuru Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa ufadhili huo na kueleza kuwa hatua hiyo ni matokeo ya jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambae aliongoza vikao vya kutafuta fedha kwaajili ya ujenzi wa Reli ya Kiwango cha SGR.

Mkurugenzi Mkuu wa TRC Masanja Kadogosa ameeleza kuwa wakati mkataba huo wa ufadhili kwa awamu ya pili ya mradi ukisainiwa, maandalizi ya kuanza kwa uendeshaji wa SGR kati ya Dar Es salaam na Dodoma yanaendelea vizuri na kuwa kazi katika vipande vingine vya awamu ya kwanza inaendelea.