Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

TRC YAANZA HATUA ZA UJENZI WA RELI ZA MIJINI


news title here
17
September
2026

Shirika la Reli Tanzania (TRC) limefanya kikao cha kwanza na mshauri mwelezi kampuni ya SYSTRA kutoka Ufaransa, inayotarajiwa kufanya upembuzi yakinifu (Feasibility Study) ya mradi wa reli za mjini (Monorail) Jijini Dar Es Salaam.

Kikao hicho kilichofanyika Septemba 17, 2026 Jijini Dar Es Salaam, ni kiashiria cha kuanza matayarisho ya mradi huo unaolenga kuboresha usafiri wa umma na kupunguza msongamano wa magari katika jiji hilo la biashara.

Katika wasilisho lake kampuni ya SYSTRA, imesema utafiti huo utabainisha mahitaji ya ujenzi wa mradi, njia itakapopita reli, teknolojia itakayotumika katika ujenzi, gharama pamoja na mfumo unaofaa katika utekelezaji wa ujenzi.

Mradi huo wa ujenzi wa reli moja, unalenga kukabiliana na ongezeko la mahitaji ya usafiri linalotokana na ukuaji wa Jiji la Dar es Salaam, ambapo kufikia 2030 inatarajiwa kuwa na Idadi ya watu wapatao milioni kumi (10).

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya wasilisho la kampuni ya SYSTRA kuhusu hatua hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Mhandisi Machibya Shiwa, amesema, “kuanza kwa mchakato huu ni hatua muhimu katika maandalizi ya kujenga mfumo wa kisasa wa usafiri wa Mijini. Upembuzi yakinifu utatupatia msingi wa kitaalamu wa kubaini namna bora ya kutekeleza mradi kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi na ukuaji wa jiji la Dar es Salaam.”

Mha.Machibya, ameongeza kuwa TRC katika ujenzi huo wa reli hiyo TRC itashirikisha sekta binafsi ili kuongeza mitaji, teknolojia na utaalamu.

“Tunatarajia ushiriki wa sekta binafsi katika mradi huu, kwa kuwa ushirikiano huo utasaidia kuleta mitaji, ubunifu na teknolojia katika ujenzi na uendeshaji wa miundombinu ya kisasa ya usafiri” amesema Mha.Machibya.

Reli hiyo inatarajiwa kupunguza muda na gharama za safari pamoja na msongamano wa magari na kuwawezesha wananchi kufika kwa urahisi kwenye maeneo ya kazi, biashara na huduma.

Kwa mujibu wa Mhandisi Shiwa, kiuchumi, mradi huo utaongeza ufanisi wa biashara, kufungua fursa za ajira na uwekezaji na kuongeza thamani ya maeneo yanayohudumiwa na reli na kupunguza hasara zinazotokana na muda unaopotea katika foleni.

‘’Hii yote ni juhudi za serikali katika kuimarisha usafiri wa mijini ukiendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga miundombinu ya kisasa na kuwezesha ukuaji endelevu wa miji na uchumi wa Taifa’’ amemalizia Mkurugenzi Mkuu huyo wa TRC