Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​TRC KUKAMILISHA UKARABATI WA MIUNDOMBINU YA RELI GODEGODE


news title here
14
January
2021

Shirika la Reli Tnzania – TRC kukamilisha ukarabati wa miundombinu ya reli katika eneo la Godegode Mpwapwa jijini Dodoma kutokana na uharibifu wa miundombinu ya reli katika eneo hilo kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo tofauti ya nchi, hivi karibuni Januari 2021.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Bi. Amina Lumuli amekagua kazi ya ukarabati katika eneo la Godegode na kueleza kuwa “Miundombinu ya reli iliyoharibika imetokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika baadhi ya maeneo ikiwemo vijiji vya Kibakwe, Kagwa, Mgoma na Mlima Wota“

Bi. Amina aliongeza kuwa eneo lenye urefu wa Mita 46 miundombinu ya reli iliondolewa na maji pia lipo eneo lenye urefu wa Kilomita 1.5 ambalo miundombinu ya reli ilifunikwa na mchanga na kupelekea kusimamisha huduma kwa muda ili kuhakikisha mafundi wanafanya kazi ya kurudisha miundombinu ya reli.

Msimamizi wa Ukarabati katika eneo hilo, Mhandisi Faraja Yusto emesema kuwa “Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kujenga tuta ili kubadilisha uelekeo wa maji ili kazi iweze kuendelea na baadaye miundombinu ya reli kurejeshwa kwa kuweka tuta na reli”

Aidha, kazi ya ukarabati wa miundombinu katika eneo hilo imekamilika kwa kiasi kikubwa na inatarajiwa muda wowote treni zitaanza kupita, ambapo zitaanza kupita treni ya majaribio ya mizigo na baadaye huduma za treni za abiria zitaendelea kama ilivyokuwa awali.

Shirika linaomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza pia shirika linaendelea na jitihada za kuhakikisha suluhisho la kudumu linapatikana ili kuondokana na changamoto hizo, halikadhalika Wananchi wanaombwa kuacha kufanya shughuli za kibinadamu karibu na maeneo ya reli kwa kuwa shughuli hizo kwa kiasi kikubwa zimekuwa zikisababisha maji kukosa uelekeo na kuharibu miundombinu ya reli.