Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

RELI YA KISASA KIPANDE CHA TANO MWANZA ISAKA KUANZA UJENZI HIVI KARIBUNI


news title here
08
January
2021

Ujenzi wa reli ya kisasa – SGR kipande cha tano Mwanza – Isaka kuanza hivi karibuni mara baada ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) na ubia wa kampuni mbili za Kichina ‘China Civil Engineering Construction Corporation’ (CCECC) na ‘China Railway Construction Corporation’ (CRCC) kutiliana saini mkataba wa ujenzi wa reli kwa kipande hicho, Chato Geita Januari 08, 2020.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Mhe. Wang Yi wameshuhudia mkataba huo ukisainiwa kati ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Ndugu Masanja Kungu Kadogosa na Mtendaji wa Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) Bwana Zhang Junle.

Ujenzi wa Reli ya kisasa kipande cha Mwanza – Isaka ni sehemu ya ukamilishaji wa awamu ya kwanza ya mradi wa SGR kutoka Dar es salaam hadi Mwanza yenye jumla ya kilomita 1219, ambapo ujenzi wake umegawanyika katika vipande vitano (5) ambavyo ni Dar es salaam - Morogoro kilomita 300, Morogoro - Makutupora kilomita 422, Makutupora - Tabora Kilomita 371, Tabora – Isaka kilomita 162 na kipande cha tano Isaka - Mwanza chenye urefu wa kilomita 341, hata hivyo Kipande cha kwanza na cha pili ujenzi unaendelea vizuri huku kipande cha kwanza kikiwa mbioni kukamilika.

Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameipongeza kampuni ya CCECC kwa kushinda zabuni hiyo ya ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Mwanza hadi Isaka yenye urefu wa Kilomita 341

“Naipongeza Kampuni ya Kichina kwa kushinda zabuni ya ujenzi wa reli ya kisasa Kilomita 341 kutoka Mwanza hadi Isaka, mradi una gharama ya Trilioni 3.0677 Fedha za kitanzania, nina matumaini watafanya kazi kubwa” alisema Mhe. Dkt. Magufuli

Aidha, mkataba uliosaniwa ni wa miezi thelathini na sita (36) na thamani ya mradi ni Shilingi za kitanzania Trilioni 3.0677. Fursa zitakazopatikana ni ajira, malighafi na vifaa vya ujenzi ambapo ajira za moja kwa moja zinakadiriwa kuwa 15,000 na zisizo za moja kwa moja ni 75,000 na malighafi za ujenzi ni saruji na nondo ambapo saruji itakayotumika inakadiriwa kuwa kiasi cha mifuko 2,500,000.

Mheshimiwa Wang Yi ameeleza kuwa “Maendeleo ya haraka ni lazima ujenge barabara na miundombinu mingine ya usafirishaji na ndio hilo tumelifanya katika maendeleo ya nchi yetu na tunategemea jitihada anazozifanya Rais Magufuli zitaleta matunda ambayo sisi tumeweza kuyapata huko china”

Mkurugenzi Mkuu wa TRC katika maelezo yake ameishukuru Serikali ya awamu ya Tano kwa kuliwezesha Shirika katika kutoa huduma na kusimamia miradi.

“Huu ni muendelezo katika ujenzi wa reli ya kisasa, tulitangaza Tenda na makampuni ya kimataifa zaidi ya 18 yalijitokeza ambapo kampuni ya CCECC na CRCC walishinda Kandarasi , tunaishukuru serikali yako kwa kutupa uhai Shirika la Reli” alisema Ndugu Kadogosa

Naye Muwakilisha wa Kampuni ya CCECC Bwana Chang Ching Lain ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuipa kampuni hiyo kazi ya ujenzi wa reli ya kisasa, ameongeza kuwa wanaahidi kutekeleza mradi huo kwa weledi na kutumia rasilimali zilizopo Tanzania ikiwemo wafanyakazi na kukamilisha mradi kwa wakati ili kuleta manufaa kwa watanzania.

Shirika la Reli linatoa wito kwa watanzania kuchangamkia na kushiriki fursa zitakazopatikana katika mradi huu mkubwa.